Kwa nini Singida United itashuka daraja

Friday February 21 2020

Kwa nini Singida United itashuka daraja,Ligi Kuu Bara,Singida United,Ligi Kuu ,timu za Ligi Daraja la Kwanza,FDL,

 

By Charles Abel

ANGALIA msimamo wa Ligi Kuu Bara. Unaiona Singida United ilipo? Ndio inayoburuza mkia kwa sasa na ni muda mrefu ipo kwenye nafasi hiyo tangu ilipoipokea Ndanda.

Wauza Alzeti

SINGIDA United inashika mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 11 ilizokusanya katika jumla ya michezo 23 iliyocheza hadi sasa. Imeibuka na ushindi katika mechi mbili tu, ikitoka sare tano na kupoteza michezo 16 hadi sasa na imebakiza jumla ya michezo 15 tu mbele yake.

Ikumbukwe kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu msimu huu, jumla ya timu nne zilizoshika mkia katika msimamo yaani kuanzia ile ya 17, 18, 19 na 20 zitashuka daraja moja kwa moja huku mbili ambazo ni zile zilizoshika nafasi ya 16 na 15 zitacheza mechi za mchujo dhidi ya timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL)

Kwenye makaratasi na kimahesabu ya soka, Singida United ina nafasi ya kubakia Ligi Kuui ikiwa itapata ushindi katika mechi zake zote zilizobakia, itavuna pointi 45 ambazo zikiunganishwa na 11 ilizonazo sasa, jumla itakuwa na pointi 56 ambazo hadi sasa ni Simba tu iliyoweza kuzivuka.

Hata hivyo, kiuhalisia na namna ligi ilivyo, labda iokolewe na maajabu tu lakini ina dalili zote za kuwa miongoni mwa nne ambazo zitashuka moja kwa moja na makala haya yanajaribu kuainisha sababu kadhaa ambazo ndizo zinachangia timu hiyo itashuka daraja ingawa maajabu yanaweza kutokea.

Advertisement

Ubutu wa washambuliaji

Huwezi kufanya vizuri katika ligi kama hauna timu inayoweza kufunga mabao ya kutosha na hilo ni tatizo ambalo linaigharimu Singida United hadi ikajikuta ipo mkiani mwa msimamo wa ligi.

Timu hiyo imefunga mabao 12 tu ikiwa ni wastani wa bao 0.5 katika kila mchezo.

Safu mbovu ya ulinzi

Unawezaje kubaki Ligi Kuu ukiwa na safu ya ulinzi ambayo inaruhusu bao katika kila mchezo huku tatizo hilo likionekana kuota mizizi kadiri muda unavyosogea mbele?

Safu dhaifu ya ulinzi kwa kiasi kikubwa inachangia kuimaliza Singida United hadi kujikuta ikiwapa mwanya wapinzani kupata ushindi dhidi yake na ndio timu ambayo imefungwa idadi kubwa ya mabao. Nyavu zake zikitikiswa mara 35 ikiwa ni wastani wa bao 1.5 katika kila mchezo.

Matokeo yasiyoridhisha nyumbani

Kwa timu ambazo zinapigania kubaki Ligi Kuu, moja ya mbinu za kufanya ni kuhakikisha zinapata ushindi katika mechi za nyumbani jambo ambalo ni tofauti kwa Singida United.

Imekuwa haifanyi vizuri ugenini lakini pia ni kibonde nyumbani ambako imepata ushindi mara moja tu, ikitoka sare mara mbili (2) na kupoteza michezo minane (8).

Unyonge kwa washindani wake

Ushindi dhidi ya timu unayoshindana nayo una faida mbili ambapo licha ya kuongeza pointi pia unasaidia kuipunguza kasi kwa kuinyima fursa ya pointi zake kuongezeka.

Singida United ilitakiwa kuhakikisha inavuna pointi kiasi cha kutosha kwa timu ambazo inawania nazo kubaki Ligi Kuu lakini matokeo yake imekuwa kinyume kwani pointi 23 zimepotea dhidi ya washindani wake kwa kufungwa ama kutoka nao sare.

Ratiba ngumu

Singida United imebakiwa na mechi saba (7) ugenini na mechi ambazo imebakiza katika uwanja wake wa nyumbani n nane (8) ambazo inatakiwa kuibuka na ushindi ili iweze kujitetea na kubakia Ligi Kuu.

Hata hivyo, mechi hizo zilizobakia kwa Singida United sio lelemama na isipojipanga vyema inaweza kujikuta ikipoteza idadi kubwa ya mechi hizo hasa zile za ugenini lakini pia hata za nyumbani.

Mechi za ugenini ilizobakiza ni dhidi ya Alliance, Simba, JKT Tanzania, Azam FC, KMC, Yanga na Ruvu Shooting wakati mechi nane ilizobakiza nyumbani ni dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union, Mtibwa Sugar, Lipuli FC, Mbeya City, Kagera Sugar, Biashara United na Tanzania Prisons.

Advertisement