Kurasini sasa wataka ubingwa wa Afrika

Dar es Salaam. Baada ya timu ya Kurasini Heat kuifunga Oilers kwa pointi 76-59 katika fainali ya Ligi ya Taifa ya Kikapu (NBL), kocha wa timu hiyo, Shendu Mwangalla amesema kitakachofuata kwa sasa ni kubeba ubingwa wa Afrika.

Mashindano ya Ligi ya Taifa yalimalizika juzi usiku kwenye Uwanja wa Don Bosco, Upanga, kwa Kurasini Heat kutwaa taji hilo.

Mwangalla aliyeleta mafanikio kwa kipindi kifupi kwa timu hiyo, alisema ubingwa waliotwaa ulitokana na maandalizi mazuri waliyofanya yakianzia kwenye mashindano ya RBA.

“Sasa kama tumebeba ubingwa wa RBA na NBL kwa nini tusibebe ubingwa wa Afrika,” alihoji Mwangalla.

Akizungumzia mchezo wa fainali dhidi ya Oilers, alisema licha kushinda mchezo wao na Oilers, timu hiyo iliwazidi katika robo mbili za kwanza, hali iliyofanya wajipange upya katika katika robo ya tatu na ya nne.

Kocha wa Vijana, Robert Manyerere aliipongeza Kurasini Heat kwa mafanikio yao ya muda mfupi ya kutwaa mataji mawili makubwa.

Katika mchezo huo wa fainali, timu ya Oilers ilianza mchezo kwa kuongoza kwa pointi 16-15, 19-19, hadi mapunziko Oilers ilikuwa mbele kwa pointi 35-34.

Robo ya tatu, Kurasini Heat walikuja juu na kufanikiwa kuongoza kwa pointi 23-13, 19-11.

Katika mchezo huo, Amin Nkosa aliongoza kwa kufunga pointi 20 akifuatiwa na Herve Mbaya, aliyefunga pointi 15 na kwa upande wa Oilers alikuwa Evance Davis aliyefunga pointi 15.

Hata hivyo, kivutio kikubwa kilikuwa kwa Maxweel Ngonga raia wa Zambia, ambaye katika mchezo huo alionekana kuwa mchezaji pekee aliyewasumbua Kurasini Heat.

Katika mchezo wa wanawake, DB Lioness iliifunga JKT Stars kwa pointi 55-54.