Kuondoka kwa Zahera Yanga kumeacha somo

Wednesday November 6 2019

Kuondoka - Zahera- Yanga -kumeacha -somo-uongozi - klabu- soka - Yanga SC-Mashabiki-Mwanasport-MwanaspotiGazeti-MwaspotiSoka-

 

Jana, uongozi wa klabu ya soka ya Yanga uliachana na kocha wake Mwinyi Zahera baada ya kuifundisha kwa mwaka mmoja na nusu.

Hatua hiyo ya Yanga imekuja siku mbili baada ya timu hiyo kutolewa katika michuano ya kuwania Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa mabao 3-0 na Pyramid ya Misri katika mchezo wa marudiano uliofanyika Jumapili iliyopita huko Cairo. Katika mechi ya kwanza iliyofanyika wiki iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Yanga ilifungwa pia kwa mabao 2-1.

Kuna msemo ajuadi wa wanamichezo usemao, makocha wanaajiriwa ili kufukuzwa. Hiyo pengine inatokana na ukweli mchezo wa mpira wa miguu kama ulivyo mingine ni wa wazi, kila mtu anafuatilia na kuona kwa macho yake. Hakuna pa kujificha na hilo ndilo lililomkumba Zahera, kocha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Mashabiki na pengine viongozi wa Yanga wamekuwa wakilalamikia mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika Ligi Kuu hasa msimu huu licha ya kuwa imecheza mechi chache.

Hata ushiriki wake katika michuano ya kimataifa, licha ya timu hiyo kongwe nchini ilishtukizwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua za awali na kufanikiwa kuvuka raundi ya kwanza kabla ya kuingia katika mchezo wa mchujo wa kuwania kuingia katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, mashabiki wake walikuwa wakilalamikia kiwango kilichokuwa kikionyeshwa na wachezaji wake uwanjani.

Wachezaji hao ambao kwa kuangalia wasifu wa kila mmoja, ni wa viwango vya juu, walitokana na mapendekezo ya Kocha Zahera mwenyewe na benchi lake la ufundi ambalo pia uongozi wa Yanga umelitupia virago jana.

Advertisement

Muunganiko wa timu na matokeo uwanjani ndivyo vilivyomponza Zahera kwani mashabiki na viongozi hawaridhishwi na mwenendo wa sasa wa kikosi hicho.

Ukiachilia mechi za kimataifa, msimu huu Yanga imeshacheza mechi nne na kati ya hizo imeshinda mbili, imefungwa moja na kutoka sare moja hivyo kujikusanyia pointi saba.

Aidha, katika mechi hizo imeshinda mabao matano lakini imeruhusu mabao manne hivyo kuibua shaka kutoka kwa mashabiki inaweza kuwa mpinzani wa kweli dhidi ya mtani wake wa jadi, Simba ambayo imeshajikusanyia pointi 21 katika mechi nane ilizocheza ikishinda saba na kupoteza moja huku ikiwa na hazina kubwa ya mabao 16 na kuruhusu matatu tu.

Kwa kuwa uamuzi wa kumwondoa au vinginevyo ni wa viongozi waliopewa dhamana na wanachama wa klabu hiyo kuisimamia na kuhakikisha inafikia malengo waliyojiwekea, sisi tunatumia fursa hii kumtakia kila la heri kocha huyo katika maisha yake nje ya klabu hiyo.

Pamoja na kutofikia malengo, tunaamini uongozi na mashabiki wa Yanga wataendelea kukumbuka na kuenzi mchango wa hali na mali wa kocha huyo hasa katika msimu uliopita ambao klabu hiyo ilipitia katika wakati mgumu kifedha.

Kwa jinsi alivyosimama kidete kuhamasisha michango kutoka kwa wanachama na mashabiki ili timu hiyo isiadhirike huku akihakikisha inatoa ushindani mkubwa katika Ligi Kuu Bara, ni mambo ambayo yataendelea kukumbukwa katika duru za soka nchini.

Baada ya kuachana na Zahera, uongozi wa Yanga umemteua Charles Boniface Mkwasa kuongoza benchi la ufundi kwa wiki mbili wakati ukiangalia kocha sahihi atakayekabidhiwa jukumu la kuisimamia timu hiyo.

Tunautaka uongozi wa Yanga kutulia na kutafakari kwa makini kabla ya kumtangaza kocha mpya.

Tunasema hivyo tukitahadharisha kwamba ikiwa itachagua kocha kwa kufuata upepo au mkumbo, haitakuwa na matokeo mazuri na itaishia kubadili walimu kila mara badala ya kujikita kwenye mipango mingine ya maendeleo ya klabu.

Katika hili, tunazikumbusha pia klabu zote za mpira wa miguu ngazi mbalimbali nchini kuhakikisha kwamba zinatumia nguvu kubwa kutafuta makocha wenye weledi na kuwakabidhi majukumu yote ya kiufundi ili wanaposhindwa kukidhi matakwa kusiwe na visingizo wakati wa kuwachukulia hatua.

Mpira ni mchezo wa hadharani, matokeo yanapokuwa mabaya kila mpenzi wa mchezo huo anaona na kwa teknolojia ya sasa, ni rahisi kubaini uwezo wa timu na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja uwanjani hivyo hakuna mahali pa kocha aliyepewa dhamana kujificha.

Hata hivyo, angalizo letu ni kwamba wakati tukiwabebesha mzigo huo makocha, hatuna budi kuhakikishamba uongozi unatimiza wajibu wake ipasavyo.

Ukishampata kocha na kumkabidhi majukumu, umpe malengo na umwezeshe kuyafikia.

Miongoni mwa mambo ya kuzingatia ni kumwacha awe huru kuonyesha uwezo wake ili pale atakaposhindwa kusiwe na malalamiko aliingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Tukijikita katika hili, tutakuwa na makocha watakaokuwa wanafanya kazi zao kitaaluma badala ya kuwa wasimamizi wa mazoezi na hiyo maana yake ni kwamba watahakikisha wanasajili wachezaji watakaowapa matokeo chanya, watakaoonyesha kiwango kizuri cha mchezo na jumla wa hayo yote ni kuongezeka kwa kiwango cha soka letu.

Katikati ya mwezi huu dirisha dogo la usajili litafunguliwa.

Tunaamini timu zote zitatumia fursa hiyo kufanya marekebisho madogo madogo ya baadhi ya nafasi ambazo zimepwaya katika vikosi vyao.

Wito wetu kwa viongozi, wahakikishe wanatoa fursa kwa makocha kutimiza wajibu wao kitaaluma ili timu zao zinapofanya vibaya wasipate wa kumsukumia mzigo wa visingizio.

Imani yetu ni kwamba Zahera alipewa kila aina ya msaada, akasajili wachezaji wazuri lakini kile kilichokuwa kimetarajiwa hakikuonekana.

Hilo liwe somo kwa timu zote hususan zile zinazoshiriki katika ligi mbalimbali. Ziwape makocha malengo ili wawajibike kwayo.

Advertisement