Koscielny asema kina Aubameyang wanazingua

Monday January 14 2019

 

LONDON, ENGLAND.LAURENT Koscielny amekataa kupepesa macho na kuwaangushia jumba bovu washambuliaji wa Arsenal kuwa ndio chanzo cha kuchapwa 1-0 na West Ham United kwenye mchezo wa Ligi Kuu England juzi Jumamosi.

Beki huyo wa kati alirudi kwenye kikosi cha Arsenal baada ya kuwa mgonjwa siku za karibuni, lakini alishuhudia kikosi chake kikishindwa kupata ushindi ugenini kwenye ligi tangu mwezi Novemba mwaka jana.

Ukweli ni kuwa Arsenal haikuonekana kabisa kama inaweza kufunga na iliteseka sana kwenye mechi hiyo ya wababe wenzao wa London. Na beki, Koscielny hakutaka kuficha mambo akisema washambuliaji wamehusika.

Alisema: “Nadhani pale kwenye eneo la kushambulia tulihitaji kuwa watulivu zaidi na kujaribu kutumia mipira tuliyopata kiufasaha zaidi. Tulipata nafasi na tumeshindwa kufunga. Ni ngumu kushinda mechi kama hufungi. Tunahitaji kuwa na mipango, tutumie vyema mipira tunayopata.”

Kocha Unai Emery alitumia fomesheni ya 3-4-3, ambapo kwenye safu yake ya washambuliaji kulikuwa na mastaa watatu Pierre-Emerick Aubameyang, Alex Iwobi na Alexandre Lacazette.

Kwenye mechi hiyo, Arsenal ilijaribu mara kadhaa lakini ilionekana kukosa utulivu ilipokuwa kwenye goli la wapinzani wake na hilo ndilo analolizungumzia Koscielny ambalo limewaponza na kupoteza mechi hiyo.

Advertisement

Bao pekee lililofungwa na Declan Rice liliamua matokeo ya mechi hiyo na hivyo Arsenal imeshindwa kuitishia amani Chelsea kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Advertisement