Kocha wa Samatta afyatuka

Muktasari:

“Hivyo sina budi kukubaliana na hali halisi, Ninafurahia mafanikio yake, ni jukumu letu kurahisisha zoezi lake la kuondoka.”

GENK, UBELGIJI .KOCHA wa Genk, Hannes Wolf amevunja ukimya kuhusiana na ishu nzima ya usajili wa mshambuliaji wake, Mbwana Samatta anayekaribia kutua katika klabu ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England.

Wolf alikuwa hajazungumza lolote tangu ishu ya nahodha huyo wa Taifa Stars kutua Villa Park ilipoanza na baada ya kimya kirefu, juzi aliamua kufunguka na kueleza msimamo wake katika suala hilo.

Kocha huyo ambaye alijiunga Genk Novemba mwaka jana na kumuongoza Samatta katika mechi tisa tu, amesema kuwa alipofika Genk aliambiwa kuwa Samatta atauzwa karibuni hivyo alijiandaa kwa hilo.

“Kamwe huwezi kunisikia ninalalamika kuhusiana na ishu ya usajili ya Ally (Samatta),” alisema Wolf. “Katika usaili wangu wa kwanza Genk niliambiwa kuna uwezekano akaondoka.

“Hivyo sina budi kukubaliana na hali halisi, Ninafurahia mafanikio yake, ni jukumu letu kurahisisha zoezi lake la kuondoka.”

Samatta ambaye amefunga mabao 76 katika mechi 191 akiwa na Genk aliyojiunga nayo Januari 2016 akitokea TP Mazembe ya DR Congo, anatarajia kukamilisha usajili wake katika kikosi cha Aston Villa kwa dau la Pauni za Uingereza 8.5 milioni.