Kocha wa Kenya aanika kikosi cha kuivaa Msumbiji, Kahata nje

Monday September 30 2019

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya.  Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, Francis Kimanzi ametangaza kikosi cha mwisho cha Stars kitakachocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Msumbiji huku akimtema kiungo wa Simba ya Tanzania, Francis Kahata.

Kwa muda mrefu Kahata amekuwa kiungo katika kikosi cha Stars, tangu alipojiunga na Gor Mahia akitokea Thika United, lakini tangu atimkie Simba SC, kiwango chake hakijawa sawa ambapo zaidi ya michezo minne ya Ligi Kuu ya Tanzania, amejikuta akianzia benchi.

Mbali na Kahata wachezaji wengine waliotemwa na Kimanzi kipa namba moja Stars, Patrick Matasi ambaye huenda nafasi yake langoni ikachukuliwa na Otieno au Shikhalo.

Katika kikosi hicho kitakachoshuka dimbani Oktoba 13, ugani Moi Kasarani pia amewarejesha kikosini Nahodha wa zamani wa Gor Mahia, Harun Shakava ambaye kwa sasa anaichezea Nkana FC ya Zambia na Anthony Akumu wa Zesco United.

Aidha, Kimanzi ameamua kuwaita baadhi ya Nyota waliosahaulika katika uongozi wa Kocha mfaransa Sebastien Migne, akiwemo mlinda lango Ian Otieno wa Red Arrow ya Zambia na mkali wa mabao ya Zesco FC, Jesse Jackson Were.

Safu ya ushambulizi itakuwa chini ya miguu salama ya Michael Olunga, Jesse Were na Masomo Juma. Safu ya kiungo itaongozwa na Nahodha Victor Wanyama akisaidiwa na Nahodha wa Gor Mahia, Kenneth Muguna.

Advertisement

Beki ya Stars itakuwa chini ya uongozi wa Harun Shakava, Joseph Okumu na Joash Onyango. Kikosi cha Stars kinatarajiwa kuripoti kambini Oktoba saba, tayari kwa mpambano huo.

Kikosi kamili cha Stars:

Makipa: Ian Otieno (Red Arrow, Zambia), Timothy Odhiambo (Ulinzi Stars, Kenya), Faruk Shikalo (Young Africans, Tanzania)

Mabeki: Johnstone Omurwa (Wazito, Kenya), Harun Shakava (Nkana, Zambia), Joash Onyango (Gor Mahia, Kenya), Yusuf Mainge (FK Pohronie, Slovakia), Hillary Wandera (Tusker, Kenya), Erick Ouma (Vasalunds IF, Sweden), Joseph Okumu (IF Elfsborg, Sweden), Samuel Olwande (Kariobangi Sharks, Kenya)

Viungo: Anthony Akumu (Zesco United, Zambia), Abdallah Hassan (Bandari, Kenya), Kenneth Muguna (Gor Mahia, Kenya), Duke Abuya (Kariobangi Sharks, Kenya), Victor Wanyama (Tottenham Hotspurs, England), Cliffton Miheso (Gor Mahia, Kenya), Lawrence Juma (Gor Mahia, Kenya), Cliff Nyakeya (FC Masr, Egypt), Whyvone Isuza (AFC Leopards, Kenya)

Mastraika: Michael Olunga (Kashiwa Reysol), Jesse Were (Zesco United, Zambia), Masud Juma (JS Kabylie, Algeria)

 

Advertisement