Kocha mpya, posho mpya Yanga

YANGA imeanza upya kila kitu. Sasa ni kocha mpya na posho mpya kwa mastaa. Yaani kila pointi 15 ambazo wataweka kibindoni kuanzia sasa kwa mechi tano mfululizo wachezaji watalamba Sh50 milioni.

Mwanaspoti limejiridhisha kwamba kocha mpya, Cedrick Kaze atatua nchini Jumatano na amethibitisha hilo. Katika misimu kadhaa ya nyuma ukiwamo uliopita wa Ligi Kuu Bara, mabosi wa Yanga walitenga Sh10 milioni fedha walizokuwa wakipewa wachezaji mara timu tu wanapomaliza mechi na ushindi.

Lakini msimu huu wamekuja kivingine kwa kutengeneza mfumo unaowatia hamasa zaidi wachezaji kuhakikisha wanashinda mechi tano mfululizo na kudakishwa Sh 50 milioni.

Walichofanya mabosi wa GSM, wadhamini wa klabu hiyo walipiga hesabu na kuona kwamba msimu mzima timu yao itakuwa na mechi 34 ambazo kama watashinda zote watavuna pointi 102. Akili yao ni kwamba kwa kima cha chini ili wawe katika ramani ya ubingwa angalau wawe na pointi 90 wakipiga hesabu kwamba watani zao Simba msimu uliopita walimaliza na pointi 88.

HESABU ZILIVYO

Ili mastaa wa Yanga wapate posho asilimia 100 ambazo ni Sh50 milioni, lazima washinde mechi tano mfululizo ambapo hizo ni pointi 15 bila kujali wapo nyumbani au ugenini. Akili ya viongozi ni kupata mafanikio kwa klabu zaidi kuliko kuangalia maslahi zaidi kwa wachezaji ambao tayari wanakuwa na mishahara mizuri.

Mpaka sasa kikosi hicho kimeshinda mechi nne kati ya tano na kutoka sare moja, hivyo kukusanya pointi 13 sawa na ilizonazo Simba iliyo juu yao kwa uwiano wa mabao yaa kufunga na kufungwa. Kwa ushindi wa mechi ya mwisho dhidi ya Coastal Union tena mnono ambao walikuwa hawajawahi kuupata msimu huu, iliwahakikisha wachezaji kudaka Sh40 milioni, ikiwa ni matokeo ya mechi hiyo na zile za ushindi dhidi ya Mbeya City, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar na sare ya Tanzania Prisons.

Kwa mujibu wa viongozi wa Yanga, hesabu zinaanza upya kwa mechi tano za awali ikiwemo dhidi ya Simba Novemba 7 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Mechi nne za awali ambazo kina Mukoko Tonombe, Carlinhos, Tuisila Kisinda, Michael Sarpong, Yacouba Songne na nyota wengine wa klabu hiyo watakazoanza kucheza kusaka Sh50 milioni ni ile ya Polisi Tanzania itakayopigwa Oktoba 22 na KMC ya Oktoba 25.

Nyingine ni dhidi ya Biashara United itakayopigwa Oktoba 31 na ile ya Gwambina FC itakayopigwa Novemba 3 kabla ya timu kurejea Dar kuikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkapa chini ya Kaze.

WASIKIE GSM

Taarifa ya mabadiliko ya posho ilithibitishwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said aliyesema yanalenga kuhakikisha timu inafanikiwa badala ya kuwapa mafanikio wachezaji kwa mchezo mmoja.

“Tunataka kuona klabu inafanikiwa katika malengo yake ya msimu, tulikuwa na mgawanyo uliopita nadhani mnakumbuka lakini hatukufanikiwa, lakini safari hii tunataka kuona tunapata mafanikio ya msimu kama klabu na sio kuwaangalia wachezaji pekee,” alisema.

“Tumezungumza na wachezaji na kila kitu kipo sawa, mwanzo waliona kama ni kitu kigumu, lakini sasa wameshakubaliana kwa vile wamegundua ubora wa kutafuta ushindi katika kila mchezo wanao. Kuna watu wanaona timu yetu inapiga sana mipira mbele ndio, ni wachezaji wakitaka kupata ushindi zaidi na pia wakiwa na ubora wa kuhakikishwa hawafungwi.”