Kocha Yanga ataka kummaliza mwarabu Dar

Muktasari:

Pyramids inayoshika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Misri ikicheza mechi tatu na kukusanya alama saba nyuma ya vinara Al Ahly yenye alama 9, ina baadhi ya nyota wanaoichezea timu ya Taifa ya Misri akiwamo kipa Ahmed El Shenawy aliyesajiliwa akitokea Zamalek, nahodha Abdallah El Said, kiungo Nabil Emad, pia ina fowadi matata Eric Traore kutoka Burkina Faso, Mtunisia Amor Layouni na fowadi kutoka Ecuador, Jhon Cifuente. Pia ina Mghana mkali John Antwi na Lumala Abdu kutoka Uganda.

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Yanga ina kibarua kigumu kama inataka kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya usiku wa jana kutupwa mikononi mwa Pyramids FC ya Misri.

Yanga iliyong’olewa Ligi ya Mabingwa ya Afrika na Zesco United ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-2 imepangwa kuvaana na klabu hiyo iliyoasisiwa mwaka 2008 na inayoshiriki michuano hiyo ya kimataifa kwa mara ya kwanza msimu huu.

Kwa mujibu wa droo iliyofanyika jana mjini Cairo, Misri, Yanga itaanzia nyumbani dhidi ya wapinzani wao hao kama ilivyokuwa kwenye hatua kama hiyo mwaka 2016 na 2018, ambapo mara zote ilifanikiwa kushinda na kutinga makundi.

Mwaka 2016 ilicheza na GD Sagrada Esperanca ya Angola na kuwafunga 2-0 jijini Dar es Salaam kabla ya kulala 1-0 ugenini, kisha ikarudia tena mwaka 2018 ikiwafumua Welayta Dicha ya Ethiopia pia 2-0 nyumbani na kulala 1-0 ugenini na kutinga makundi.

Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi pengine Yanga ingetupwa kwa timu za nchi jirani, wawakilishi hao walipangwa na Pyramids inayonolewa na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Uganda, The Cranes, Sebastien Desabre.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Yanga itawakaribisha wapinzani wao hao ambao rekodi zinaonyesha wamekuwa na matokeo mazuri kwenye mechi za ugenini katika mechi ya kwanza itakayiopigwa Oktoba 27 kabla ya kurudiana nao Novemba 3.

Kwa mechi za nyumbani, Pyramids hawatabiriki kwani katika mechi zao za awali hadi kutinga playoff, waliwanyoosha Etoile du Congo ya Congo Brazzaville kwa mabao 4-1 nyumbani na kushinda ugenini 1-0, kisha kutoka sare ya 1-1 na CR Belouizdad ya Algeria na kwenda kuwanyoosha kwao bao 1-0 na kufuzu hatua ya playoff.

Awali, timu hiyo ilifahamika kama Al Assiouty Sport, ilianza kucheza Ligi Kuu ya Misri mwaka 2014 na mwaka jana ilinyakuliwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Michezo ya Saudia, Turki Al Sheikh na kubadilishwa jina kuwa Pyramids kabla ya Julai 4, mwaka huu mfanyabishara wa Falme za Kiarabu, Salem Al Shamsi kuimiliki kwa kuwa na hisa nyingi.

Pyramids inayoshika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Misri ikicheza mechi tatu na kukusanya alama saba nyuma ya vinara Al Ahly yenye alama 9, ina baadhi ya nyota wanaoichezea timu ya Taifa ya Misri akiwamo kipa Ahmed El Shenawy aliyesajiliwa akitokea Zamalek, nahodha Abdallah El Said, kiungo Nabil Emad, pia ina fowadi matata Eric Traore kutoka Burkina Faso, Mtunisia Amor Layouni na fowadi kutoka Ecuador, Jhon Cifuente. Pia ina Mghana mkali John Antwi na Lumala Abdu kutoka Uganda.

Pia, ni klabu ya tatu kwa utajiri barani Afrika nyuma ya Al Ahly na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. Katika kikosi chake msimu huu, Pyramids imefanya usajili wa bei mbaya ikiwemo kumnunua straika Mbrazili, Marcos Da Silva au Keno kwa Sh20 bilioni kisha ikampeleka kwa mkopo klabu ya Al Jazira ya Saudi Arabia.

Hata hivyo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila amewataka Wanayanga kutokuwa na presha na kama watautumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo, basi mchezo wa marudiano hautakuwa mgumu.

“Nimeiona ratiba sio ngumu wala sio rahisi, lakini naamini kama tutatumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri yenye mabao mengi basi, ugenini tunakwenda kumaliza kazi mapema,” alisema Mwandila.

Kikosi cha Mwinyi Zahera kilipenya hatua hiyo baada ya kuing’oa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1, wakitoka nao sare ya 1-1 nyumbani na kushinda ugenini 1-0 huku walitoshana nguvu ya 1-1 na Zesco United nyumbani na kulala ugenini 2-1 baada ya kiungo wake fundi wa mpira, Abdulaziz kujifunga alipokuwa akiokoa mpira.