Kocha Machester City apewa fungu la usajili, kuvuta wanne kwa mpigo!

Tuesday May 14 2019

 

London, England. Manchester City imepanga kutumia Pauni 200 milioni kwa usajili wa majira ya kiangazi.

Kocha Pep Guardiola anatarajiwa kupewa fungu hilo baada ya kuipa Man City ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya pili mfululizo.

Guardiola anataka kujenga kikosi imara na tayari ana orodha ya nyota wanne anaowataka ambao ni Rodri, Luka Jovic, Matthijs De Ligt na Houssem Aouar.

Kocha huyo anataka beki, viungo wawili na mshambuliaji ambao anaamini watakuwa chachu ya mafanikio ya Man City msimu ujao.

Kiungo wa Atletico Madrid, Rodri anawindwa kwenda kuongeza nguvu kwa mkongwe Fernandinho, ambaye mwezi huu anatimiza miaka 34.

Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo, Txiki Begiristain alikwenda kumuangalia Rodri, mwenye miaka 22 na thamani yake inatajwa ni Pauni 60 milioni.

Advertisement

Man City inamtolea macho mshambuliaji wa Frankfurt Luka Jovic, pia kinda wa Benfica Joao Felix mwenye miaka 19.

Jovic, mwenye thamani ya Pauni 50 milioni, anawindwa na klabu nyingi ikiwemo Real Madrid.

Pia Guardiola anavutiwa na kiwango cha beki wa kati wa Leicester City Harry Maguire na kiungo mkali Houssem Aouar wa Lyon aliyecheza kwa kiwango bora katika Ligi ya Mabingwa Ulaya mechi za makundi.

Nicolas Otamendi, Fabian Delph na Eliaquim Mangala ni miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kutupiwa virago.

 

Advertisement