Kocha Azam ageukia ufundi

Muktasari:

  • Kikosi cha Azam kilianza mazoezi mnamo Mei 26 mwaka , baada ya serikali kutangaza kuruhusu shughuli za michezo kurejea baada ya kusimama kwa muda kama tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona.

KIKOSI cha Azam leo kimeendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa Kiporo wa Ligi Kuu Tanzania bara dhidi ya Mbao FC unaotarajiwa kupigwa tarehe 14 ya mwezi huu katika dimba la Azam Complex, saa 1.00 usiku huku benchi lake la ufundi likionekana kuyapa kipaumbele mazoezi ya ufundi na mbinu.

Katika mazoezi hayo ambayo yalianza majira ya saa 16:05, chini ya kocha msaidizi Bahati Vivier,  Azam walifanyia kazi zaidi mazoezi ya mbinu na ufundi kwa kuchezea mpira zaidi kuliko kufanya mazoezi ya viungo kama ilivyokuwa siku za mwanzoni.

Mazoezi hayo yalikuwa na vipindi vitatu, baada ya kuanza kuanzia saa 16:05 jioni hadi saa 16:20 jioni wachezaji wakapumzika, kabla ya kuingia kwenye kipindi cha pili ambacho kilianza saa 16:24 jioni na mwisho kikafata  kipindi cha tatu ambacho kilianza saa 16:36 jioni hadi mwisho.

Hii ni tofauti na timu hiyo ilipoanza kujifua hapo awali ambapo walionekana kufanya mazoezi ya viungo kuliko kuchezea mpira.

 Azam walifanya mazoezi hayo huku ikiwakosa wachezaji wake Obrey Chirwa, Donald Ngoma na Razak Abarola ambao wamekwama nchini mwao kutokana na mipaka na safari za kutoka nje ya nchi kufungwa katika nchi hizo.