Klopp amshangaa Aubameyang, atamba kuwa mchezaji wake

Tuesday May 14 2019

 

LIVERPOOL, ENGLAND.JURGEN Klopp amedai kushtushwa na kwamba hakuwahi kuwaza kabisa kama Pierre-Emerick Aubameyang naye angefunga mabao ya kumfanya ashinde tuzo ya Kiatu cha Dhahabu kama walivyofanya mastaa wake Mohamed Salah na Sadio Mane.

Bosi huyo wa Anfield, ambaye alishindwa kumaliza ukame wa miaka 29 wa Liverpool kushinda taji la Ligi Kuu England baada ya kuona ubingwa huo ukinyakuliwa na Machester City, alishangaa tena kuona hata Kiatu cha Dhahabu kuna mchezaji mwingine wa kutoka timu isiyokuwa Liverpool amebeba.

Aubameyang alifunga mara mbili dhidi ya Burnley kufikisha mabao 22 na hivyo kulingana na Mane na Mo Salah ambao nao walifunga idadi kama hiyo ya mabao 22.

Klopp alisema: “Tuna wafungaji bora wawili, sivyo? Oh, Auba amefunga mara mbili tena? Huko Burnley? Wow, sijawahi kulitarajia hilo. Watafanyaje sasa, wanawatengenezea viatu vitatu? Au kila mmoja anakuwa nacho kwa miezi mitatu? Ile, wote ni wachezaji wangu, sivyo?”

Klopp alisema hivyo kwa sababu Aubameyang aliwahi kuwa chini yake wakati alipokuwa Borussia Dortmund kati ya mwaka 2013 na 2015.

Wachezaji hao wote watatu walikabidhiwa tuzo zao za ufungaji bora kutokana na kufunga mabao hayo 22 kila mmoja.

Advertisement

Advertisement