Klopp ajitetea kichapo kizito

LIVERPOOL, ENGLAND. JURGEN Klopp amesema timu yake ya Liverpool imetokea tu kuchapwa mabao saba lakini si kwamba kikosi chake ni kibovu.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England walikumbana na kipigo kizito huko Villa Park walipopigwa 7-2 na Aston Villa, huku straika Ollie Watkins akipiga hat-trick.

Jambo hilo limekuja baada ya Jumatatu iliyopita, kocha huyo kurushiana maneno na gwiji wa Manchester United, Roy Keane alipohoji uwezo wa kukaba wa timu hiyo kwenye ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Arsenal.

Klopp alisema: “Tumekosea tu mchezoni baada ya kuwa nyuma kwa 1-0. Hata hivyo, hicho hakiwezi kuwa kisingizio. Unaweza kuwa nyuma kwa 1-0 na unafanya mambo unayotaka. Tumetengeneza nafasi, lakini tulishindwa kujilinda na kila mpira tuliopoteza lilikuwa shambulio kali.

“Ukabaji wetu ulikuwa wa kawaida sana na hatuweza kurudi kwenye mchezo, kila kitu kilikataa. Tulifanya makosa mengi sana na makubwa. Ilianzia kwenye goli la kwanza na tuliendelea kufanya makosa mengine.

“Haya makosa yote yametokea kwenye mechi moja. Si kwamba timu yetu ni mbovu kama bwana Keane alivyosema.”

Liverpool haikuwa na huduma ya kipa wake namba moja Alisson kwenye mchezo huo kutokana na kuumia bega huku mastaa wake Sadio Mane na Thiago Alcantara hawakucheza kutokana na kupimwa na kukutwa na virusi vya corona.

Beki wa kati, Virgil van Dijk aliwaambia wachezaji wenzake kwamba watalazimika kutuliza akili zao kabla ya kukabiliana na mahasimu wao wakuu wa Merseyside, Everton - ambao wapo kwenye kiwango bora kabisa kwa sasa.

Van Dijk alisema: “Ni lazima tukalipiane wenyewe na inapaswa kuwa hivyo. Mbaya sana kupoteza kwa namna ile kama tulivyopoteza. Hatukuwa mchezoni tangu mwanzo kabisa na hatukupaswa kufungwa mabao mengi vile.

“Huwezi kuwaondolea sifa yao Villa, lakini tulipaswa kutumia nafasi tulizopata. Hatuwezi kuchanganyikiwa, lakini inatulazimu kubadilika.”