Kiungo Azam asaka dili la kukipiga Latvia

Friday January 24 2020

Kiungo Azam asaka dili la kukipiga Latvia-Latvia, Riga FC,  Mudathir Yahya- Azam FC,

 

By Eliya Solomon na Charity James

BAADA ya kutua Dubai kwa majaribio ya kujiunga na mabingwa mara mbili mfululizo wa Latvia, Riga FC, kiungo wa Kitanzania, Mudathir Yahya amewatoa shaka wadau na mashabiki mbalimbali wa soka nchini kwa kusema hawezi kuichezea nafasi hiyo.

Kiungo huyo wa Azam FC, hakuwepo katika kikosi cha timu yake tangu katika mchezo ambao ilicheza dhidi ya Yanga na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mudathir alisema anamshukuru Mungu kwa sababu amefika salama Dubai ambako klabu hiyo imeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Latvia ambao, unatarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi ujao, Februari.

“Nitafanya majaribio ya wiki nne. Nina imani ya kuwa nitafanya vizuri hivyo itapendeza kama dua za Watanzania zitakuwa juu yangu. Tangu nimefika mapokezi yalikuwa mazuri na walinipa muda wa kupumzika kabla ya kuanza majaribio hayo.

“Sina presha kwa sababu kwa muda ambao nimecheza soka nyumbani nimejifunza mengi ambayo naamini yatakuwa msaada katika majaribio yangu,” alisema Mudathir.

Kiungo huyo, aliongeza kwa kusema, “Klabu yangu imenipa baraka zote za kuja kufanya majaribio hivyo nikifanya vizuri bila shaka kwa mikono yote miwili wataniruhusu kuanza maisha yangu mapya ya soka Ulaya.”

Advertisement

Hii ni mara ya pili kwa mchezaji wa Kitanzania kwenda kufanya majaribio nchini humo. Juni mwaka jana, aliyekuwa mchezaji wa Yanga, Maka Edward alienda Latvia kufanya majaribio ya kujiunga na Spartaks Jurmala.

Hata hivyo, Maka hakufuzu majaribio hayo na badala yake akapata nafasi ya kujiunga na Moghreb Tetouan, inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco, aliko pia Mtanzania mwingine Saimon Msuva.

Advertisement