Kituo cha Michezo Marsh Athletic champongeza mdau wa soka

Muktasari:

  • Sylvester Marsh alifariki March 14,2015 katika hospitali ya Taifa, Muhimbili kwa saratani ya koo, ambapo katika uhai wake aliwahi kuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' ambapo leo ametimiza miaka minne tangu afariki dunia.

Mwanza. Ikiwa ni mwaka wa nne tangu aliyekuwa Mkurugenzi wa kituo cha Michezo Marsh Athletic jijini hapa, Sylvester Marsh afariki dunia leo, uongozi wa kituo hicho umekabidhi Cheti cha shukrani kwa mdau wa soka, Jamali Babu ambaye amekuwa bega kwa bega kusapoti kituo hicho.

Akizungumza wakati wa kukabidhi cheti hicho, Mwenyekiti wa kituo hicho,Maarufu Mohamed amesema kuwa kwa kutambua mchango wa mdau huyo wao kama uongozi wameamua kuandaa zawadi hiyo ili iwe kumbukumbu kwake katika sapoti yake kwenye Soka la Mwanza hususani kituo cha Michezo cha Marsh Athletes.

"Pamoja na wadau wengine,lakini huyu Babu amekuwa ni mtu pekee ambaye amekuwa pamoja na sisi wakati wote,amejitolea vitu vingi bila kuchoka,hivyo hii tuzo ni kutambua mchango wake," amesema Mohammed.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa ikiwa ni mwaka wa nne sasa tangu mwasisi wa kituo hicho afariki dunia, changamoto kubwa ni gharama za kodi ya pango kwa wachezaji na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kusapoti.

 Kwa upande Babu amesema kuwa kutokana na uongozi wa kituo hicho kutambua mchango wake bado ataendelea kuwasapoti kwani Marehemu Marsh alipenda michezo na maendeleo kwa ujumla.

"Kipekee niwashukuru viongozi wa kituo kwa kutambua mchango wangu niahidi kwamba nitaendelea kuwa na nyinyi kwani marehemu Marsh alikuwa mpenda maendeleao amesema Babu ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM (NEC).

Naye Mwakilishi wa Soka la Wanawake Mkoa wa Mwanza, Sophia Makilagi amewaomba wadau kuendelea kuyaenzi yale yote mema aliyoyaacha marehemu Marsh.

"Kwa ujumla tunaendelea kusikitika kwa kifo chake,lakini niwaombe wadau wa Soka nchini kuendelea kuenzi yale mema aliyoacha," amesema Makilagi.