Messi vs Ronaldo : Kisa kukwepa kodi, Messi ahusishwa na genge la Mafia

Muktasari:

Jorge pia alikiri dhamira ya watu hao ilikuwa kukwepa kodi kwa kutumia haki za matumizi ya picha za Messi na kujingizia fedha bila ya yeye kuhusishwa.

Katika toleo lililopita tuliona jinsi Messi alivyokuwa akihaha mahakamani kujinasua katika kashfa ya ukwepaji kodi, akisaidiwa na baba yake kujenga hoja mahakamani. Sasa endelea…

Messi alijieleza kwa namna ilivyotosha na baba yake alikuwa akimsaidia kwa kumpa baadhi ya mambo machache ya kuyasema.

“Nilijua kwamba tulikuwa tukisaini mikataba na wadhamini ambao wlaikuwa wakitoa kiwango X cha fedha na mimi nilikuwa na kazi ya kutoka hadharani, kupigwa picha na mambo kama hayo lakini sikuwa najua fedha zinakwenda wapi.’’ alisema Messi akiiambia mahakama.

Jorge (baba wa Messi) naye akathibitisha alichokisema Messi kwamba mchezaji huyo hakuwa akifahamu chochote. “Tulimpa mikataba na alichokifanya ni kuisaini tu.

Hata hivyo na kiongozi huyo wa familia naye pia akakiri tatizo lake akisisitiza kwamba aliwaamini kwa asilimia 100 wahasibu wake na kwamba wahasibu hao ndio waliounda mfumo wa usimamizi kibiashara, mfumo uliozingatia mambo ya unafuu katika kulipa kodi bila ya yeye kuhusishwa.

Jorge pia alikiri dhamira ya watu hao ilikuwa kukwepa kodi kwa kutumia haki za matumizi ya picha za Messi na kujingizia fedha bila ya yeye kuhusishwa.

Hata hivyo wakili wa Serikali hakuna alichokubali katika hayo, badala yake alimini Messi alikuwa akijua mengi kuliko ambayo amekuwa tayari kuyakiri na hapo hapo akatoa shutuma kwa namna ya kuruka.

“Sitaki kumlinganisha Messi na ‘mafioso’ (genge la mafia wa Italia wanahusishwa na makosa ya jinai) lakini ni kama vile naye alikuwa ni kinara wa genge la mfumo unaoendesha shughuli za kijinai,’’ alifafanua wakili huyo akielezea kilichoonekana kuwa ni hisia zake.

Uamuzi ulipangwa kutangazwa Julai 7, 2016 na ulikuwa kama ifuatavyo; Baba na mtoto wake wakahukumiwa kifungo cha miezi 21 jela kwa kosa la udanganyifu katika mamlaka za kodi, hukumu ambayo wanasheria wa kina Messi waliikatia rufaa.

Na wakati kesi hiyo ikiendelea kuwa mjadala, pia kulikuwa na habari nyingine isiyo ya kupendeza ambayo nayo ilikuwa ikisubiriwa na ambayo pia ingeishia mahakamani.

Jina la Messi likawa miongoni mwa majina ya kwanza kwanza kuonekana katika kashfa maarufu iliyoitwa ‘Panama Papers’.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kuhusu kashfa hiyo, Messi na baba yake walidaiwa kukuanzisha kampuni isiyo rasmi mjini Panama ambayo ilikuwa ikitimiwa kwa malengo ya kukwepa kodi zinazotokana na mauzo ya haki mbalimbali za Messi zikiwamo picha zilizotumika kwenye matangazo ya televisheni.

Baada tu ya kutoka habari hiyo, familia kwa haraka ilitoa taarifa ya kukanusha kufanya kosa lolote.

“Kampuni ya Panama ambayo imetajwa katika ripoti ni kampuni ambayo haipo hai, na ambayo haijawahi kuwa na akaunti au kupata fedha zozote na imeanzishwa kutokana na mfumo wa kampuni ya zamani ambayo ilianzishwa na washauri wa masuala ya fedha wa zamani wa Messi.

“Mambo yote kuhusu uwepo wa kampuni hiyo yameshawekwa sawa ikiwamo fedha ambazo zilikusanywa kutokana na haki za matangazo za Messi kabla na baada ya kufanyika taratibu nyingine za kimahakama, vyote vimewekwa wazi katika mamlaka za usimamizi wa kodi za Hispania.”

Baada ya hapo kilichofuata ni kwa mamlaka za usimamizi wa fedha Hispania kuanza uchunguzi wa tuhuma zilizowekwa wazi na Panama Papers, ukweli kuhusu hilo haukuweza kuthibitishwa.

Yote kwa yote sifa na hadhi ya Messi ikawa kama imetingishwa kwa mara nyingine kuhusu utata huo wa mambo ya fedha ukihusisha ukwepaji wa kodi.

Itaendelea Jumanne ijayo…