Kisa corona:Kocha ahofia usalama wa kambi Simbu, Failuna Kenya

Muktasari:

Simbu na Failuna ni wanamichezo pekee nchini waliofuzu kushiriki Olimpiki inayotarajiwa kuanza Julai 26 nchini Japan wakichuana katika mbio ndefu za barabarani (marathoni).

Dar es Salaam.Kocha Thomas Tlanka wa wanariadha Failuna Abdi na Alphonce Simbu amesema kambi ya wanariadha wa Olimpiki nchini Kenya haitokuwa salama kwao.

Kambi hiyo ambayo awali ilipangwa kuanza Aprili Mosi uenda ikachelewa ili kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Corona unaotikisa dunia.

Tayari ugonjwa huo umeingia katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki ikiwamo Kenya na Tanzania, Uganda, na Rwanda huku nchi hizo zikifunga mipaka yake kuzuia watu kuingia.

Akizungumza na tovuti ya Mwanaspoti, kocha Tlanka alisema kama itafika Mei pasipo kambi hiyo kuanza, basi haitakuwa salama kwa wanariadha hao kujiunga nayo tena.

Alisema ikitokea wakachelewa kuanza kambi hiyo hadi Mei, itawaathiri wachezaji katika kubadili hali ya hewa.

"Kitaalamu walipaswa kwenda miezi mitatu kabla ya mashindano ya Olimpiki, lakini mpaka sasa haijajulikana wataanza lini kambi hiyo na haijulikani janga la Corona litakwisha lini.

"Ikitokea imefika Mei na hawajafanikiwa kwenda kwenye hiyo kambi, ni heri RT (Shirikisho la Riadha Tanzania) likawaaacha waendelee kujifua hapa nchini," alisema.

Alisema watakapobadili hali ya hewa na kwenda Kenya kwa namna moja au nyingine wataanza upya na ndani ya muda mfupi hawatoweza kuzoea mazingira na hali ya hewa ya kule, kisha wajifue kwa kiwango bora kwa ajili ya Olimpiki," alisema.