Kisa corona: Wachezaji wa Simba SC kukatwaa mishahara

Muktasari:

Simba inatumia Dola za Kimarekani 100,000 (zaidi ya Sh230 milioni) kwa mwezi kulipa mishahara na masuala mengine ya msingi kwa wachezaji, benchi la ufundi na waajiri wengine gharama gharama hizo zipo palepale.

Dar es Salaam.Wachezaji wa Simba SC huenda wakakatwa mishahara yao endapo Ligi Kuu Tanzania Bara itasimama kwa muda mrefu kutokana janga la ugonjwa wa corona.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amesema wajumbe wa bodi bado hawajajadili uwezekano wa kuwakata sehemu ya mshahara wachezaji wao ili kuchangia jamii katika janga la corona au kubana matumizi.

“Huko nje wenzetu wamekubaliana kukata mishahara kwa wachezaji na makocha kwa vile wana vyanzo vingi vya mapato kama haki za matangazo ya TV, wadhamini wengi pia,” amesema Senzo

Senzo amesema kwamba licha ya kuwa ligi imesimama kupisha mlipuko wa ugonjwa wa corona, lakini gharama za kuendesha timu zipo palepale kama awali wakati ligi ikiwa inaendelea.

Senzo amesema walikuwa wanatumia Dola za Kimarekani 100,000 (zaidi ya Sh230 milioni) kwa mwezi kulipa mishahara na masuala mengine ya msingi kwa wachezaji, benchi la ufundi na waajiri wengine gharama gharama hizo zipo palepale.

“Gharama zinaendelea kuwa juu kwa kutumia pesa zile zile kama Dola 100,000 kwa mwezi wakati huohuo tukikosa vyanzo vyetu vya msingi vya kuingiza pesa ambazo hutupunguzia gharama na matumizi yetu,” alisema mtendaji huyo raia wa Afrika Kusini.

“Tunakosa pesa za viingilio uwanjani, mauzo ya jezi na vifaa vya timu uwanjani, ni jambo ambalo linasababisha tunakosa kipato, lakini wadhamini wetu wanakosa muda wa kuwatangaza maana shughuli nyingi za kuwatangaza zimesimama.

“Kama uongozi tunaendelea kujipanga na kutafuta vyanzo vya mapato ili kuendesha shughuli za timu katika kipindi kigumu ambacho dunia inapitia,” alisema Senzo ambaye tayari ameshaanza kushughulikia ishu za usajili.