Kisa Micho, Chama afunguka

Muktasari:

Micho amesema wachezaji hao wameonyesha utovu wa nidhamu baada ya kushindwa kujiunga na wenzao licha ya kukatiwa tiketi za ndege mara mbili.

BAADA ya kocha wa timu ya Taifa Zambia, Milutin Sredojević 'Micho' kutangaza kwamba hajafurahishwa na nidhamu ya wachezaji wanaocheza Ligi ya Tanzania, Clatous Chama (Simba) na Obrey Chirwa (Azam Fc) kuchelewa kujiunga na timu ya Taifa licha ya kutumiwa tiketi za ndege tangu Jumatatu.

Kauli hiyo imemuibua winga wa Simba, Clatous Chama kuonyesha hisia zake kwa kuandika katika ukurasa wake wa Instagram, kwamba hajakosa ndege mara mbili kama ambavyo inaelezwa.

"Ukweli ni kwamba sijakosa ndege zote mbili, niliongea na mwalimu kabla hata ya mechi yetu na Dodoma na nilimuelezea kwamba haitokuwa rahisi mimi kupanda ndege ya kwanza kwa sababu ilikuwa saa tatu asubuhi Jumatatu na sisi tulicheza Jumapili saa kumi jioni, umbali wa kutoka Dodoma mpaka Dar ni masaa nane, pia timu ilikuwa hairudi Dar baada ya ile mechi" aliandika Chama.

Chama aliandika zaidi akisema tiketi ya pili aliipata jana (Jumanne) na muda wa kuondoka ukiwa ni saa 8:45 usiku, wakati nikiwa najiandaa na safariniliambiwa sitakiwi kusafiri.

"Sikubaliani na Wazambia wengi wanaoamini kwamba sina nidhamu, Lakini mimi sijakosa ndege zote mbili ambazo nilikatiwa tiketi,Ahsanteni sana na naitakia mazuri Zambia".

Awali Micho alisema "Kama mtu anatoka Russia na anafika Zambia inakuaje huyu ambaye tupo nae katika mipaka ya karibu? hii sio nidhamu nzuri na sitokubali kuiona mtu akiwa juu zaidi ya Taifa".

Kwa upande wa mshambuliaji Obrey Chirwa wa Azam FC nao mechi yao ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar ilichezwa Jumapili usiku hapa hapa jijini Dar es Salaam.