Kipigo cha Yanga kina maswali mengi kwa Zahera

Muktasari:

Kwa matokeo hayo, Yanga inalazimika kuibuka na ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ugenini ili isonge mbele na kutinga hatua ya makundi, vinginevyo itaaga rasmi mashindano hayo.

Aprili 20, 2016 Abdallah El Said alikwamisha ndoto za Yanga kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifungia bao la pili timu ya Al Ahly ya Misri lililoifanya iibuke na ushindi wa mabao 2-1 ikiwa nyumbani jijini Cairo.

Yanga ikidhani mechi hiyo itakwenda kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam kumalizika kwa sare ya bao 1-1, El Said alitumia vyema udhaifu wa safu ya ulinzi ya Wanajangwani kufunga bao la kichwa ambalo liliwatupa nje Yanga kwenye mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Miaka mitatu na nusu baadaye, Abdallah El Said kwa mara nyingine amehusika katika kuiweka Yanga kwenye mazingira magumu ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuipachikia bao la pili timu yake ya Pyramids FC iliyoibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-1 ugenini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ikiwa ni mechi ya kwanza ya hatua ya mchujo ya mashindano hayo huku timu hizo zikipangwa kurudiana jijini Cairo, Jumapili hii.

Kwa matokeo hayo, Yanga inalazimika kuibuka na ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ugenini ili isonge mbele na kutinga hatua ya makundi, vinginevyo itaaga rasmi mashindano hayo.

Mwanaspoti liliitahadharisha Yanga

Siku chache kabla ya mchezo huo, Mwanaspoti na gazeti lake dada, Mwananchi yaliipa tahadhari Yanga kuhusu nyota watano tishio kwenye kikosi cha Pyramids FC ambao inapaswa kuwachunga zaidi.

Kundi hilo la nyota watano linaongozwa na El Said, washambuliaji John Antwi na Mohamed Farouk, winga Eric Traore na kiungo Ibrahim Hassan.

Kati ya wachezaji hao watano, ni watatu tu ambao walianzishwa kwenye kikosi cha kwanza na wawili kati yao, El Said na Traore ndio walioifungia mabao hayo mawili yaliyoifanya Pyramids FC kuibuka na ushindi huo mzuri wa ugenini.

Pengine Yanga haikuwatilia maanani nyota hao na kuwafuatilia kisha kuandaa mpango mkakati wa kuwadhibiti ili wasilete madhara kama walivyofanya juzi Jumapili.

Usajili, maandalizi vilizingatia mahitaji?

Lakini hilo linaweza kuwa sababu ndogo tu iliyochangia kilichoikuta Yanga juzi dhidi ya Pyramids lakini dalili zake zilianza kuonekana mapema.

Aina ya usajili na maandalizi ambayo Yanga ilifanya kwa ajili ya msimu huu vilileta hofu ya mapema kwa wadau wa soka nchini juu ya ushiriki wa timu hiyo kwenye mashindano ya kimataifa.

Hakukuwa na uwiano mzuri katika usajili ambao Yanga iliufanya ambapo kwenye baadhi ya nafasi walijaza kundi kubwa la wachezaji huku nafasi nyingine zikiwa na upungufu.

Matokeo yake benchi la ufundi likawa linalazimika kuwapanga wachezaji kwenye nafasi ambazo sio zile wanazocheza kiasili pindi wahusika wanapokuwa majeruhi au wanatumikia adhabu, jambo lililopunguza ufanisi wao ndani ya uwanja.

Mfano, mabeki wa kati waliosajiliwa na Yanga msimu huu ni saba lakini hapohapo wana beki mmoja tu asilia anayecheza nafasi ya beki wa kushoto.

Kana kwamba haitoshi, ikifahamu fika ugumu wa mashindano ya kimataifa, Yanga ilijikita katika kucheza mechi za kirafiki dhidi ya timu dhaifu ambazo zilishindwa kuanika udhaifu ilionao na kinyume chake ikawa inazifunga idadi kubwa ya mabao ambayo yaliihadaa na kuifanya ijione imekamilika.

Upangaji wa kikosi & mbinu

Kama kuna eneo ambalo linaonekana kuiumiza Yanga msimu huu ni mbinu ambazo imekuwa ikizitumia katika mechi mbalimbali pamoja na upangaji wa kikosi.

Wakati timu ikionekana kuwa na tatizo kubwa kwenye safu ya ushambuliaji ambayo ni wazi imekuwa ikihitaji kuwa na ufanisi wa hali ya juu ili iweze kupachika mabao, benchi la ufundi la Yanga kipaumbele chake kimekuwa zaidi kwenye safu ya kiungo ambayo limekuwa likijaza idadi kubwa ya wachezaji na kuifanya iwe na idadi ndogo ya wachezaji kwenye eneo la adui pindi inaposhambulia.

Kwa bahati mbaya, kati ya washambuliaji wanne ambao imewasajili, ni mmoja tu ambaye kiasili anaweza kusimama kama mshambuliaji wa mwisho naye ni David Molinga ambaye hata hivyo hana kibali cha kutumika kwenye mashindano ya kimataifa wakati wengine ni aina ya wachezaji ambao kiasili wanamudu vilivyo kucheza nyuma ya straika wa kati.

Lakini pamoja na kujaza idadi kubwa ya wachezaji kwenye safu ya kiungo, bado Yanga imekuwa ikizidiwa umiliki wa mpira kwenye idadi kubwa ya mechi, jambo linalofanya ijiweke kwenye hatari ya kuwapa mwanya wapinzani wao kutengeneza nafasi na kulifikia lango lao kirahisi.

Kingine kinachoonekana kuigharimu Yanga ni kutopewa nafasi kwa baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa wakifanya vizuri pindi wanapopangwa katika nafasi fulani.

Ilianzia kwa Juma Abdul anayecheza nafasi ya beki wa kulia ambaye licha ya kuonekana yupo fiti, benchi la ufundi la Yanga lilikuwa likimsotesha benchi na badala yake kuwapanga Ally Ally au Seleman Mustafa ambao sio mabeki wa pembeni kiasili.

Lakini pia huku likifahamu fika kuwa David Molinga hatumiki kwenye mashindano ya kimataifa, benchi la ufundi la Yanga limekuwa likimpa nafasi mara kwa mara ya kucheza huku likishindwa kufanya hivyo kwa Juma Balinya ambaye anatumika kwenye mashindano hayo.

Hilo limethibitishwa na nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi ambaye amefichua kuwa anashindwa kuonyesha kiwango bora kutokana na benchi la ufundi la Yanga kumpanga katika nafasi ambayo haimudu.

“Nikicheza namba sita huwa nafanya vizuri zaidi, lakini kwa kuwa kocha anaamua anichezeshe namba 10 siwezi kukataa kwani mimi nipo kwa ajili ya kucheza ingawa siwezi kufiti sana.

“Mpira una mambo mengi unaweza kuona upo sahihi kila unapopangwa, lakini walio nje ya uwanja wanaona tofauti na kukukosoa. Sipendi nicheze chini ya kiwango, napenda kuonekana bora kila mara, sipendi kuonekana natumia fedha za timu vibaya.

“Kocha ndiye anajua kwa nini mchezaji anachezeshwa nafasi gani kwa wakati gani. Kikubwa ninachoweza kusema mimi nafiti nafasi ya kiungo na ndiyo niliyokuwa naicheza tangu nimejiunga na Yanga. Kwasasa siwezi kumsemea mwalimu kwanini ananipanga namba hiyo,” alisema Tshishimbi.

Hata hivyo, Zahera ameonyeha kuwa tofauti na nahodha wake kwa kudai kuwa kiungo huyo anatimiza sifa za msingi za mchezaji anayecheza kwenye nafasi anayompanga sasa.

“Mnaposema hachezi vizuri nawashangaa. Mimi kile ninachomwambia akifanye akiwa katika nafasi hiyo ndicho anachokifanya. Namuweka pale nikiwa na maana kwamba anatakiwa kupiga mipira ya mwisho vizuri ikiwa ni sambamba na kufunga mwenyewe akipata nafasi ya kufunga.

“Na kumchezesha namba kumi haina maana kwamba anatakiwa kukaa katika eneo moja. Anaweza akatoka kwenda kusaidiana na viungo kupandisha mashambulizi. Kikubwa ni kuhakikisha anarudi kwenye eneo lake kwa wakati ili aweze kukamilisha majukumu mengine,” alisema Zahera.

Kuhamisha Uwanja kumeisaidia Yanga?

Zikiwa zimebaki wiki mbili kabla ya mechi ya juzi dhidi ya Pyramids FC, Yanga ilitangaza uamuzi wa kupeleka mchezo huo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Katika hali ya kushangaza, Yanga ilifanya mazoezi katika siku zisizozidi saba kwenye uwanja huo, na kujinyima nafasi ya kuuzoea kiasi cha kutosha na haikushangaza kuona ikishindwa kucheza aina ya soka ambalo imelizoea na kulazimika kuingia na staili tofauti ili kuendana na mazingira ya eneo la kuchezea la uwanja huo.

Kipa Farouk Shikalo alionekana angeweza kuokoa goli lile la kwanza, lakini mpira ulidunda kwenye ‘tuta’ la uwanja mbele yake na kumchenga na kutinga wavuni.

Ninja, Chambua wafunguka

Beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye kwa sasa anakipiga LA Galaxy ya Marekani, alimshauri kocha Mwinyi Zahera kutowaanzisha wachezaji wapya zaidi ya watano katika mechi moja kwa madai bado hawajazoea Ligi Kuu Bara.

Ninja alisema hana maana kwamba wachezaji wapya waliosajiliwa ni wabovu isipokuwa anaona wanatakiwa kupewa muda wa kuzoea hali halisi ya ligi ilivyo.

“Ninachoona kinaweza kumsaidia Zahera ni kuwachanganya wachezaji wapya na wazawa hapo ndipo wanapoweza kuanza kukaa kwenye mstari ama kupata kombinesheni nzuri ambayo itawafanya wafanye maajabu msimu huu,” alisema.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema Yanga haina straika wa kufosi mashambulizi na kushauri wakati wa usajili wa dirisha dogo anahitajika mdunguaji wa aina ya Meddie Kagere wa Simba.

“Ukisema timu ipo kwenye kiwango utambue unazungumzia safu ya ushambuliaji ambayo inasaka pointi kila mechi, ninachokiona ni Yanga hitaji la kusajili kupitia dirisha dogo mtu ambaye atakuwa anafosi mashambulizi,” alisema.

Zahera akwepa lawama

Kocha wa Yanga, Mkongomani Mwinyi Zahera alisema mpaka wanaingia katika mchezo huo wa juzi alikuwa ameshawapatia wachezaji wake kila kitu ambacho wanacho timu pinzani kwa maana aina yao ya kucheza katika kukaba na kushambulia.

Zahera alisema aliwasoma wapinzani wao na kufahamu wanatumia pasi nyingi za chini ila katika mechi ambayo wanacheza viwanja vigumu kama CCM Kirumba Mwanza huwa wanabadilisha aina yao ya uchezaji na kucheza mipira mirefu ya juu.

“Ikanilazimu kumtumia Abdulaziz Makame, kutokana na urefu wake na umahiri wa kucheza mipira ya juu lakini katika mpango wangu wa kwanza kama wapinzani wangecheza mpira wa chini asingeweza kuanza katika kikosi cha kwanza,” alisema.

“Sikutaka kumtumia Makame kutokana na uwezo wake wa kushindana ulikuwa chini tangu ametoka katika timu ya Taifa, na nafasi ya kiungo tulipanga kumtumia Feisal Salum na Kabamba Tshishimbi huku katika eneo la ushambuliaji Sadney Urikhob na Juma Balinya.

“Akili yangu ilifanikiwa kwa Makame kwenda kucheza mipira mingi ya vichwa na kuzuia safu ya ulinzi kufikiwa mara kwa mara na kama angekosekana tungeweza kufungwa mabao mengi zaidi ya hayo mawili kwani wachezaji wengi wa timu pinzani walikuwa warefu.

“Nilizisoma mbinu za kocha wa timu pinzani kutokana nilikutana naye tukiwa kwenye Afcon wakati huo akiwa na timu ya taifa ya Uganda. Anaweza kufunga mabao kupitia mipira ya juu kama si kona basi friikiki na kupampanga Makame tulifanikiwa na hata mabao ambayo tulifungwa ni makosa madogo ya bahati mbaya ambayo yanatokea katika mchezo wowote,” alisema Zahera.

“Kama tumepoteza katika mechi ya nyumbani sioni sababu ya kwenda kuzuia katika mechi ya marudiano kwani tutakwenda kwa kushambulia na tukiamini kupata matokeo mazuri kutokana katika mechi zote ambazo tumecheza za mashindano haya tumefunga bao ugenini,” aliongezea Zahera.

REKODI YANGA

Lakini wakati Zahera akiyasema hayo, udhaifu wa safu ya ushambuliaji ya Yanga katika kufumania nyavu msimu huu kulinganisha na msimu uliopita, unaleta shaka juu ya uwezekano wa wawakilishi hao wa Tanzania kuibuka na ushindi mnono ugenini dhidi ya Pyramids Jumapili.

Rekodi zinaonesha msimu uliopita katika mechi nne za mwanzo Ligi Kuu Bara Yanga walishinda michezo yote huku kila mmoja wakifunga zaidi ya mabao mawili.

Mechi ya kwanza Yanga walicheza dhidi ya Mtibwa Sugar na kushinda 2-1, mabao yaliyofungwa na Heritier Makambo, ambaye hayupo katika kikosi kwa sasa na Kelvin Yondani ambaye alifunga kwa mkwaju wa penalti.

Mechi ya pili waliifunga Kagera Sugar mabao 2-1, ambayo yalifungwa na Makambo pamoja na Raphael Daud. Mechi ya tatu walicheza na Mwadui ambayo nayo walishinda 2-1, mabao yakifungwa na Makambo na Mrisho Ngassa.

Mechi ya nne ilikuwa dhidi ya Stand United ambayo walishinda mabao 4-3, ambayo yaliwekwa kambani na Ngassa, Ibrahim Ajibu ambaye yupo Simba msimu huu pamoja na Andrew Vicent ‘Dante’ na Deus Kaseke.

Msimu huu rekodi zinaonesha katika mechi nne za mwanzo Yanga wamecheza wameshinda mbili, kipigo kimoja na sare 1.

CHARITY JAMES, OLIPA ASSA, YOHANA CHALLE, KHATIMU NAHEKA, THOBIAS SEBASTIAN NA CHARLES ABEL