Kichapo hakijampa shida Mkapa

Friday October 16 2020

 

By Yohana Challe

Dar es Salaam. Kocha wa Njombe Mji, Kenneth Mkapa amesema kichapo walichokipata wiki iliyopita dhidi ya Mbeya Kwanza cha bao 1-0 hakikumuumiza kichwa kutokana na maandalizi waliyofanya.

Mkapa alisema baada ya dirisha la usajili kufungwa hawakupata muda wa kuwaweka pamoja wachezaji wake kutokana na muda kuwabana tangu ligi ilipomalizika msimu uliopita.

“Tangu tuingie kambini tulicheza michezo miwili pekee ya kirafiki ikiwa wiki moja kabla ya ligi kuanza, jambo ambalo lilikuwa gumu kwetu kusema tumepata kikosi cha kwanza.

“Hadi tunaingia kwenye mchezo wa kwanza sikuwa na wachezaji wa kikosi cha kwanza, hii ilinifanya kushindwa kujua nimtumie nani kwa wakati gani kwenye mchezo ule,” alisema Mkapa.

Aliongeza kuwa baada ya kupoteza mchezo huo wamejipanga na kuboresha mapungufu yaliyojitokeza.

Njombe Mji itakuwa Uwanja wa Sokoine, mkoani Mbeya kucheza na Boma FC, ambayo katika mchezo wake wa kwanza iliichapa Gipco FC bao 1-0 lililofungwa na mkongwe, Gaudence Mwaikimba.

Advertisement

Timu hiyo ilipanda Ligi Kuu msimu wa 2017/18 na kudumu kwa msimu mmoja kisha kurudi tena FDL.

 

Advertisement