Kibira amwachia Mungu kuenguliwa Chaneta

Muktasari:

Kibira aliyekuwa akitetea nafasi yake kwenye uchaguzi uliofanyika leo Jumamosi alienguliwa kwenye usaili uliofanyika Ijumaa mjini Dodoma.

Dar es Salaam. Saa chache baada ya Anna Kibira kuenguliwa kwenye usaili wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), mwenyekiti huyo aliyemaliza muda wake amesimulia chanzo cha kuenguliwa kwake.

Kibira aliyekuwa akitetea nafasi yake kwenye uchaguzi uliofanyika leo Jumamosi alienguliwa kwenye usaili uliofanyika Ijumaa mjini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja alisema kwamba Kibira ataendelea kuwa mjumbe wa heshima wa Chaneta.

"Tumemuengua Kibira kwa kuwa tumeona hataweza mikiki mikiki ya netiboli kutokana na afya yake," alisema Kiganja.

Akizungumza sakata hilo, Kibira alisema alichofanyiwa anamuachia Mungu.

"Yote nimeamua kumwachia  Mungu, najua ilipangwa iwe hivyo, nitaendelea kutoa mchango wang Chaneta pale itakapohitajika," alisema Kibira.

Nafasi ya Kibira sasa ilikuwa ikiwaniwa na Dk Devotha John na Damian Chonya kwenye uchaguzi huo.

Kibira ameongoza Chaneta katika kipindi mmoja cha miaka minne akichukua nafasi ya Anna Bayi.