Kiapo cha baba na mama chamkimbiza Khabib ulingoni

Muktasari:

Khabib aliugumia maumivu makali wakati akitangaza kustaafu mchezo huo.

Uchungu wa mzazi ajuaye mwana. Ni msemo waliotuachia wahenga, ukilenga umio la mzazi kwa mtoto wake.

 

Msemo huo umekuwa na maana iliyoumiza kwa bondia mkali wa ngumi mchanganyiko, Khabib Nurmagomedov, aliyetangaza kustaafu mchezo huo kwasababu ya kumpoteza baba yake mzazi Abdulmanap Nurmagomedov.

 

Ndio. Mzee Abdulmanap alifariki katikati ya janga la covid-19,  Mei mwaka huu na kumuachia majonzi makubwa Khabib kutokana na ukweli kwamba mzee huyo ndio alikuwa kocha wake.

 

Ni sababu hiyo ya kufariki kwake, ndio imemfanya Khabib aamue kustaafu kabisa kucheza ngumi mchanganyiko (mixed martial arts) zinazosimamiwa na kamisheni ya UFC, chini ya Rais Dana White.

 

Khabib alitangaza uamuzi huo ulioshtua wengi muda mfupi tu baada ya kumtandika mpinzani wake Justin Gaethje kwenye raundi ya pili usiku wa kuamkia lei Oktoba 25, 2020.

 

Gaethje aliyekuwa anashikilia mkanda wa mpito baada ya kumpiga Tony Ferguson mapema mwaka huu, na kufanikiwa kukata tiketi ya kupigana dhidi ya Khabib.

 

Ni matakwa hayo ya kupigana na Gaethje ndio yaliyomlazimu Khabib apigane kutetea mkanda wake aliokuwa anaushikilia wa lightweight.

 

Ndivyo ilivyokuwa, raundi mbili tu zilitosha kumfanya Khabib ampige Gaethje kwa Knockout (KO) na akapiga magoti chini akaweka kichwa chake kwenye mikono na kulia akitokwa machozi makali ya hisia kuugulia maumivu ya kumpoteza baba yake Abdulmanap.

 

Sio hivyo tu. Khabib hatimaye alifichua kiapo ambacho alimpatia mama yake aliyetaka asipigane tena hata dhidi ya Gaethje lakini akamuahidi kwamba huo ndo utakuwa wa mwisho, hivyo hatarejea tena kupigana kwa heshima ya baba yake mpenzi na aliyekuwa kocha wake mkuu.

 

Wakati anatangaza uamuzi huo, Khabib anaacha rekodi yake tamu ya kushinda mapambano yote 29 bila kupoteza wala sare, ambayo hata hivyo angeweza kuiongeza kama sio kuamua kustaafu kuheshimu kiapo na ahadi aliyompatia mama.

 

Kama sio kustaafu, Khabib alikuwa kwenye kusubiri mshindi wa pambano kati ya Conor McGregor dhidi ya Dustin Poirier ili apigane naye.

 

Mabondia wote wawili hata hivyo kwa nyakati tofauti walishachapwa na Khabib ambaye wakati anatangaza uamuzi huo alisema pia haoni umuhimu wa kuwasubiri kwasabu alishawapiga.

Staa Cristiano Ronaldo amempongeza kwa uamuzi huo na kumwandikia kwenye mtandao wa Instagram kuwa "Baba yako atajivunia kwa hili" huku McGregor akimpongeza kwa pambano lake na kusema ataendeleza mchezo huo kisha kumalizia kwa kutoa salamu za pole kwa familia yake.

 

Kwa wapenzi wa ngumi mchanganyiko, uamuzi wa Khabib ni pigo kuu kutokana na umwamba aliokuwa nao ulingoni (octagon) jina linalotumika kwenye mchezo huo.