Kesi ya Malinzi yapigwa kalenda hadi kesho

Muktasari:

  • Kesi ya Utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa (TFF) Jamal Malinzi na wenzake imeshindwa kuendelea na ushahidi baada ya Hakimu, Maila Kasonde anayeendesha shauri hilo kupata udhuru.

Dar es Salaam. Kesi ya Utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa (TFF) Jamal Malinzi na wenzake imeshindwa kuendelea na ushahidi baada ya Hakimu Maila Kasonde anayeendesha shauri hilo kupata udhuru.

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alidai kuwa amepata taarifa hakimu Kasonde anayeendesha shauri hilo amepata udhuru.

Swai alidai kuwa shauri lilikuja kwa aliji ya kusikiliza hivyo ameiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine. Hakimu Augustina Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 25 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Washitakiwa wengine ni Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga ambao wakikabiliwa na mashitaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani, 375,418.

Miongoni mwa mashitaka hayo ni inadaiwa, katika mashitaka ya kwanza kuwa Juni 5, mwaka jana, maeneo ya jiji la Dar es Salaam, Malinzi na Selestine walighushi nyaraka ya maazimio ya kamati tendaji ya Juni 5, mwaka jana kwa lengo la kuonesha kuwa kamati hiyo ya TFF imelenga kubadili mtia saini wa shirikisho hilo katika akaunti za benki kutoka Edgar Masoud kwenda kwa Mwanga.