Kesi ya Aveva: Mahakama kutoa uamuzi wa kupokea nyaraka za TBS zikiomba kufutiwa kodi Simba

Muktasari:

Shahidi hiyo aliendelea kudai kulikuwa na nyaraka kutoka klabu ya Simba zilizoambatanishwa na hati ya kiwanja pamoja na barua zilizowasilishwa TBS zikiomba kuondolewa kodi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Agosti 28 mwaka huu kutoa uamuzi wa kupokea kielelezo katika kesi ya kugushi na kutakatisha fedha inayomkabili aliyekuwa rais wa Simba, Evans Aveva na wenzake.

Mbali na Aveva, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Makamu wa wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Wakili wa utetezi Nehemiah Nkoko alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba kuwa nyaraka kutoka TBS zinazotaka kuwasilishwa na upande wa mshitaka kama kielelezo hazijakidhi matakwa ya kisheria.

Nkoko alidai hayo baada Mchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Frank Mkilanya (45) kuwasilisha nyaraka kutoka Simba kwenda TBS zikiomba kuondolewa kodi.

"Nyaraka zinazotaka kuwasilisha na shahidi ili kama kielelezo hajaonyesha alizitoa wapi kutokana na sheria ya ushahidi kuelekeza unapotaka kutoa nyaraka uonyeshe risiti" alidai Wakili Nkoko

Akiongozwa na Wakili kutoka (Takukuru) Leonard Swai, Shahidi huyo alieleza ankara (invoice) iliyotumika kupelekwa mamlaka ya mapato (TRA) tofauti na iliyotumika na klabu ya Simba kununulia nyasi.

Alidai alipoenda TRA alikuta ankara ya ya Dola 40000 ambapo viongozi wa klabu ya Simba wakisema nyasi zimebunuliwa kwa dola 109499.

"Ankara (invoice) niliyoikuta TRA niliikuta ndiyo hiyo hiyo iliyowasilishwa shirika la viwango (TBS) na kukuta barua iliyosainiwa na Evansi wakiomba msamaha wa kodi" alidai Mkilanya

"Kuna garama waliomba ziondolewe walipotakiwa kuwasilisha ankara (invoice) waliwasilisha ile niliyotoa taarifa TRA baada ya kuona kuwa ankara mbili zimetumika" alidai

Mkilanya alidai TRA waliendelea na mchakato wakijua uhalisi na baadae nikasikia klabu ya Simba wamekubali kulipa kodi inayotakiwa.

Alidai kodi ambayo ingelipwa kwa kutumia ankara ya dola 40000 ingekuwa ndogo zaidi kuliko ya dola 109499 ambapo klabu ya Simba ingepata faida.

Shahidi hiyo aliendelea kudai kulikuwa na nyaraka kutoka klabu ya Simba zilizoambatanishwa na hati ya kiwanja pamoja na barua zilizowasilishwa TBS zikiomba kuondolewa kodi.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 28, mwaka hui atakapotoa uamuzi kuhusiana na kielelezo hicho.

Tayari mashahidi saba wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 10, yakiwemo ya kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uongo na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila Kamati ya Utendaji ya Simba, kukaa kikao.

Katika mashitaka la kughushi linawakabili washitakiwa wote, anadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika mashitaka mengine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.