Keown anasema Man United Top 4 wataisikia redioni

Muktasari:

  • Arsenal wao kwa upande wao watacheza na timu nyingi zilizopo kwenye sehemu za katikati ya msimamo wa ligi kama vile Crystal Palace, Watford na Wolves, lakini shida wana mechi nyingi za ugenini, ambazo ni udhaifu mkubwa kwa kikosi hicho cha kocha Unai Emery.

LONDON, ENGLAND.BEKI wa zamani wa Arsenal, Martin Keown anaamini kwamba Manchester United hawatakuwamo kwenye Top Four ya Ligi Kuu England msimu huu kwa sababu wana ratiba ngumu sana.

Badala yake, Keown anaamini timu yake ya zamani Arsenal ndiyo itakayokamatia nafasi ya mwisho kwenye ile nne bora akiziweka nje Chelsea na Man United, huku Tottenham akiwatabiria kumaliza msimu wakiwa kwenye nafasi ya tatu.

Kwenye mchakamchaka huo, Man United bado wana mechi dhidi ya Manchester City wanaoshindania ubingwa na watakuwa na kipute pia dhidi ya Chelsea ambao pia wanapambana kuwamo kwenye Top Four.

Arsenal wao kwa upande wao watacheza na timu nyingi zilizopo kwenye sehemu za katikati ya msimamo wa ligi kama vile Crystal Palace, Watford na Wolves, lakini shida wana mechi nyingi za ugenini, ambazo ni udhaifu mkubwa kwa kikosi hicho cha kocha Unai Emery.

“Nadhani Manchester United hawatakuwamo kwenye Top Four,” alisema Keown.

“Arsenal, unanitarajia mimi kusema nilichosema, lakini nikitazama ratiba yao si ngumu kama ya Man United. Ukitazama hizi mechi wakicheza na Man City, nadhani hiyo itakuwa mechi ya sare, sidhani kama watashinda. Watapata pointi 75, zitakuwa sawa na Arsenal, lakini watashindwa kwa tofauti ya mabao.”