Kenya, Tanzania ni mechi ya mashindano Afcon

Wednesday June 26 2019

 

By Said Pendeza

TUGANGE yajayo. Maneno mawili yenye uungwana mkubwa. Hayo maneno ya wahenga yanawahusu zaidi Harambee Stars na Taifa Stars kwenye mwanzo wao wa michuano ya Afcon 2019 huko Misri.

Usiku wa juzi Jumapili, Harambee Stars na Taifa Stars, majirani hawa warudi kete zao za kwanza kwenye Kundi C na kilichotokea kilitokea.

Taifa Stars walitangulia kuwakabili Senegal, kisha Harambee Stars wakacheza na Algeria baadaye. Majirani walikumbana na kipigo kinachofanana, Mbili Bila kwa kila mmoja.

Matokeo yaliyotafsiri uwezo wa timu zao kwa kujilinganisha na wapinzani waliokabiliana nao. Kwenye mechi ya Taifa Stars na Senegal, matokeo ya Mbili Bila yalikuwa na afadhali kubwa kwa Watanzania, kwa sababu walizidiwa kila kitu ndani ya uwanja.

Pengine ubao wa matokeo ungesomeka kwa namba nyingi zaidi kama washambuliaji wa Senegal wangekuwa na utulivu mkubwa walipokaribia bao la Stars, huku kipa Aishi Manula akiibuka nyota wa mchezo wa upande wa Watanzania aliwaokoa wasikumbane na aibu kubwa zaidi.

Kisha ikaja zamu ya majirani zao. Harambee Stars nyota wake walifanya makosa mechi yasiyokuwa ya lazima na hayo yaliwagharimu mbele ya Algeria, ambayo ilikuwa na wachezaji mahiri sana kwenye kikosi chao kama Riyad Mahrez.

Advertisement

Ni wazi unapocheza na wachezaji wa aina hiyo, hupaswi kufanya makosa ya kizembe, kwa sababu yatakugharimu.

Mechi hizo za kwanza zilionyesha uzito tofauti wa shuka na blanketi baina ya mataifa haya mawili ya Afrika Mashariki na yale ya Afrika Magharibi.

Safari bado ni ndefu. Sawa kwenye kikosi cha Taifa Stars kulikuwa na staa wao, Mbwana Samatta na kwenye timu ya Harambee Stars kulikuwa na Victor Wanyama.

Lakini, isingeweza kuleta tofauti kubwa kutokana na wachezaji wengine waliowazunguka mastaa hao, uwezo wao ulikuwa tofauti kabisa na wale waliokuwa kwenye vikosi vya Senegal na Algeria kwa kuwatazama mchezaji mmoja mmoja.

Haya hayo ya mechi ya kwanza yameshapita. Kujikwaa si kuanguka na sasa macho yapo kwenye mechi za pili kwenye kundi hilo.

Kitu kibaya au pengine kizuri, hatima ya kila timu kati ya Harambee Stars na Taifa Stars zipo mikononi mwao wenyewe.

Kila mmoja atajiokoa mwenyewe. Mechi ijayo, itakayopigwa Alhamisi wawili hao watamenyana wenyewe kwa wenyewe na kule kwingineko, Algeria watacheza na Senegal, nao wataumizana wenyewe kwa wenyewe.

Mechi ya Harambee Stars na Taifa Stars ina mambo mengi. Kwanza ujirani, lakini pia kufahamiana kutokana na kukutana mara nyingi.

Lakini, hii itakuwa mara ya kwanza kukutana kwenye Afcon, hivyo kila timu itakuwa na ulazima wa kutaka kuandikisha rekodi yao bora kwenye michuano hiyo walipokutana.

Hapo ndipo unapokuja utamu halisi. Ni Wanyama au Samatta nani atamtambua mwenzake. Utamu wa mchezo huu ni kwamba hautajali matokeo ya huko kwenye uwanja mwingine utakaowakutanisha Senegal na Algeria.

Mechi ya Harambee Stars na Taifa Stars ina nguvu ya pekee yake. Kila upande utahitaji kuonyesha kwamba wao ni kiboko linapokuja suala la kumenyana kwenye michuano mikubwa.

Kitu kizuri kwenye fainali za Afcon 2019 kuna timu nyingi za Afrika Mashariki na Kati zimefuzu.

Uganda wao walianza vyema kabisa wakiandikisha ushindi muhimu kwenye mechi ya kwanza mbele ya DR Congo.

Hesabu za kwenye karatasi Harambee Stars na Taifa Stars zote bado zina nafasi ya kutinga raundi inayofuata kwa kuzingatia kwamba soka imekuwa na matokeo mengi ya kikatili.

Kila timu hapo bado ina mechi mbili, huku ikizingatiwa kwamba Senegal na Algeria zitakutana zenyewe kwenye mechi ijayo.

Harambee haijacheza na Stars na Simba wa Teranga, akishinda anapenya. Stars hawajacheza na Harambee na Algeria, wakishinda zote wanapenya.

Jambo jingine zuri kuhusu fainali hizi za Afcon 2019 ni kwamba kutakuwa na timu nne kutoka kwenye makundi hayo sita ambazo zitafuzu kupitia kigezo cha best loser.

Pengine kukusanya pointi nne kwenye makundi yao, yanaweza kuwapa fursa hiyo ya kuwa miongoni mwa timu zitakazotinga hatua inayofuatia kwa kupitia best loser kitu ambacho bado kinawezekana kwa Harambee na Stars.

Lakini, yote kwa yote yatafahamika baada ya mechi yao wenyewe. Pengine hiyo itakuwa mechi ya michuano hii ya Afcon 2019 huko Misri.

Advertisement