Keane anaposimama nyuma ya Maguire

Saturday October 17 2020

 

WATU wagumu wanapita, nyakati ngumu hazipiti’ aliwahi kusema mwanafalsafa fulani hivi. Ni Kweli. Wamepita wengi. Huku katika soka wamepita wengi. Wengi sana. Mmojawapo alikuwa Roy Keane. Mgumu na jeuri mzaliwa wa Cork pale Ireland.

Roy, mgumu kama alivyo alikuwa katika injini ya maisha ya kila siku ya Manchester United. Katika kilele cha ugumu wake inadaiwa kwamba ni wachezaji wachache mno wa Manchester United waliokuwa na namba yake ya simu ya mkononi. Hawazidi sita.

Roy Keane hakuhudhuria harusi ya David Beckham. Mtu wake wa karibu uwanjani. Kila kitu kilichoendelea kuhusu Beckham na mpenzi wake Victoria Adams aliona ubishoo.

Sihitaji kukumbushwa bifu lake la kila siku na Patrick Vieira enzi hizo. Wala sihitaji kukumbusha jinsi alivyofukuzwa klabuni na Sir Alex Ferguson baada ya kujifanya yeye ni bosi zaidi klabuni kuliko kocha wake huyo Mskotishi.

Lakini juzi nilikuwa nikimtazama Keane, licha ya ukali wake wote akimponda kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate kwa kushindwa kumkumbatia na kumpiga kofi kidogo la faraja mlinzi wake, Harry Maguire aliyepewa kadi nyekundu dhidi ya Denmark. Nilijiuliza, ni keane huyuhuyu ninayemfahamu?

Keane halisi angekuwa upande wa Southgate, lakini kwa sasa hata yeye mwenyewe huruma inamshika anapogundua kwamba mwanadamu anaiyeitwa Harry Jacob Maguire anapitia wakati mgumu. Huyu ndiye mlinzi ghali kwa sasa duniani.

Advertisement

Achilia mbali pambano moja tu la juzi dhidi ya Denmark, Maguire, anapitia nyakati ngumu zilizopitiliza katika mechi za Manchester United. Kama sio kosa la kitimu basi atafanya kosa lake binafsi. Mashabiki wa timu yake na wa wapinzani wanamuandama, waandishi wa habari wanamuandama, kila kitu kinamuandama.

Kitendo cha Roy kumtetea kimenifanya nitafakari mengi kuhusu Harry Maguire. Akiwa na Hull City alikuwa ni mlinzi niliyemhusudu. Nilijiuliza kwanini timu kubwa hazimuoni? Baadaye akaibukia Leicester City ambayo walinzi wake wawili, Robert Huth na Wes Morgan walionekana kupitwa na wakati baada ya ubingwa ule wa maajabu wa mwaka 2016.

Akiwa na Leicester City hakuwahi kuwaangusha. Alikuwa nguzo. Manchester United haikutoa kwa bahati mbaya Pauni 85 milioni kuinasa huduma yake. Inawezekana pesa ilikuwa kubwa zaidi kwa sababu ya ‘Uingereza wake’. Inawezekana hakustahili hiyo pesa. Lakini bado alikuwa mlinzi mzuri.

Kitendo cha kwenda Manchester United kimerudisha nyuma maisha ya Maguire. Anapitia wakati mgumu. Nini kinamsibu Maguire? Sijui. Inawezekana kuna mambo mengi. Unaishia kukisia tu kwamba huenda kuna mambo mengi.

Kwangu, kubwa zaidi ni kwamba ameikuta timu yenyewe ipo chini. Kando yake anacheza na nani? Victor Lindelof. Huyu Mswidishi alishafeli siku nyingi kabla ya kufika kwa Maguire. Kama Maguire angecheza na Nemanja Matic au Rio Ferdinand si ajabu asingekuwa bora zaidi.

Wakati mwingine unahitaji kucheza sambamba na wachezaji bora. Wakati mwingine unahitaji kucheza katika timu bora zaidi. Si ajabu United inamuangusha. Raha ya kucheza timu bora ni kwamba huwa inawafanya wachezaji bora kuwa bora zaidi na wachezaji wa kawaida kuwa bora.

Leo, Andy Robertson sio Marcelo lakini anacheza katika timu bora ya Liverpool na inamfanya awe bora zaidi. Hivi unaamini Trent Alexander Arnold angekuwa bora katika kikosi cha Arsenal chini ya Unai Emery? Anacheza timu bora ambayo inamfanya awe bora zaidi. Kuna wachezaji wengi wa kawaida wameweza kung’ara katika timu za kawaida kwa sababu ya uwezo mkubwa wa kikosi chenyewe.

Ray Parlour hakuwa mchezaji wa ajabu lakini katika vikosi vile vya akina Thierry Henry asingeweza kukosa kung’ara.

Leo Maguire anacheza na nani kuanzia mbele mpaka nyuma? Kina nani wanaweza kumng’arisha? Jaribu kutazama pale Liverpool. Virgil Van Dijik alikuwa hitimisho la mwisho katika kikosi baada ya kikosi chenyewe kuundwa na kuanza kung’ara vilivyo.

Van Dijik anapumzishwa vilivyo na uwezo wa Liverpool kuwa na mpira muda wote. Ni muda mchache tu anaolazimika kuonyesha uwezo wake binafsi. Muda wote timu yake ina mpira.

Muda wote timu yake inamiliki mpira. Unaamini kuwa Van Dijik angekuwa Manchester United angekuwa bora kama alivyo? Unaamini Trent angekuwa bora kama alivyo kama angekuwa anachezea Everton? Sidhani.

Hapo hapo tuje katika suala la kocha. Ole Gunnar Solskajer ana uwezo wa kumfanya Maguire awe beki bora zaidi ya alivyo? Hatuna uhakika. Kuna makocha ambao wamewahi kuwafanya baadhi ya wachezaji kuwa wa hali ya juu.

Huyu Jurgen Klopp kuanzia alikotoka mpaka sasa ana uwezo wa kuwafanya wachezaji wa kawaida wawe bora. Tangu enzi za akina Mario Gotze, Shinji Kagawa, Nuri Sahin na wengineo. Halafu tunajua alichowafanya akina Sadio Mane, Mohamed Salah na wengineo pale Liverpool.

Ukigeuka kwa Pep Guardiola angalia alichofanya kwa akina Andres Iniesta, Lionel Messi, Sergio Busquets, Xavi Hernandez na wengineo. Halafu angalia alichokuja kufanya kwa akina Raheem Sterling, Kelvin de Bruyne, Bernardo Silva na wengineo.

Na sasa mgeukie Solskjaer utuambie ni mchezaji gani amemfanya kuwa bora zaidi kuliko alivyokuwa. Hapa ndipo unapomuonea huruma Maguire.

Kuna mambo mengi ambayo yanamzunguka lakini United hawakuwa wajinga kutoa zile pesa kwa Maguire. Kuna kitu walikiona ambacho sasa kimepotea kwake.

Na inawezekana kwamba kadri ambavyo tunampigia kelele na kiasi chake kikubwa cha pesa alichonunuliwa basi Maguire anazidi kupotea. Huwa inatokea katika mchezo unaoitwa soka. Huwa inatokea kwa vichwa laini kama cha kwake. Sio kila mtu anaweza kuhimili. Sio kwamba namtetea Maguire lakini naamini United hii inazidiwa kumfanya awe mchezaji wa kawaida. Ana matatizo yake binafsi lakini kuna wajinga wengi wapo sehemu nyingine wananufaika na ubora wa timu.

 

Advertisement