Kaze awafunika, Zahera, Zlatko

USHINDI iliyopata Yanga leo kwenye mchezo wao dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam umemfanya Kocha wake, Cedric Kaze kuwafunika watangulizi wake ndani ya timu hiyo akiwamo Mwinyi Zahera, Luc Eymael na Zlatko Krmpotic kwa kuanza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu kwa kishindo.

Kocha huyo kutoka Burundi, leo alikuwa akiiongoza Yanga kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo, kuchukua nafasi ya Zlatko aliyetumuliwa Jangwani Oktoba 3 na kushuhudia timu hiyo ikishinda bao 1-0 lililowekwa kimiani na kiungo Mkongoman, Mukoko Tonombe katika dakika ya 70.

Tofauti na Mwinyi Zahera aliyeanza kuinoa Yanga kumalizia mechi za msimu wa 207-2018 kwa sare kama ilivyokuwa kwa Zlatko na kipigo kwa Eymael, kocha Kaze alipata ushindi huo ulioendeleza rekodi ya Yanga msimu huu kwa kutopoteza mchezo wowote na kucheza mechi tano mfululizo bila wavu wake kuguswa na wapinzani katika ligi hiyo.

Eymael aliyetimuliwa kwa tuhuma za kutoa kauli za kibaguzi alianza ligi kwa kufumuliwa mabao 3-0 na Kagera Sugar, huku Zlatko akiianza ligi kwa sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons kama ilivyokuwa kwa Zahera ambaye alitimuliwa Novemba mwaka jana.