Kaze atoa maagizo mapya Yanga

KOCHA mpya wa Yanga, Cedrick Kaze amezungumza kwa kirefu na wasaidizi wake, Juma Mwambusi na Vladmir Niyonkuru na jana mchana timu imerudishwa kambini Kigamboni.

Kaze ambaye ni raia wa Burundi amelithibitishia Mwanaspoti kwamba anatua nchini Alhamisi saa 4 usiku na kama ni kuonana na wachezaji wake itakuwa ni Ijumaa.

Kocha huyo amesema kwamba tayari amekuwa na majadiliano ya kina na wasaidizi wake na kuwapa programu ambazo walianza nazo jana na leo kwenye tizi la asubuhi na jioni watazidi kukimbiza.

“Timu ina wachezaji wazuri sana na asilimia kubwa ya hao wachezaji wa nje ya Tanzania nimehusika kwenye usajili wao kwa kiasi kikubwa kinachohitajika kwa sasa Yanga ni kuwapa maelekezo mazuri ya kiufundi pamoja na kuhakikisha wanakuwa fiti zaidi,” aliongeza Kaze alipozungumza na Mwanaspoti kutoka Canada.

Kikosi hicho ambacho jana kiliingia kambini, kilifanya matizi chini ya Mwambusi ambaye Kaze ameonekana kumwamini zaidi kutokana na uzoefu wake na mafanikio aliyoyapata kwa kubeba kombe enzi zile akiwa na Hans Pluijm.

Kaze na timu yake wameamua kubadilisha ratiba ya mazoezi baada ya kugundua kuwa kiufundi programu ya mazoezi mara moja haina afya kwa uimara wa timu ya ushindani.

“Kweli kocha Mwambusi ataendelea na ratiba yake mpaka Ijumaa na baada ya hapo basi kocha Kaze ndio atampokea Jumamosi na Jumapili,” alisema Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli.

Lakini Kaze ambaye ni kocha mwenye leseni A ya CAF, alisisitiza Mwanaspoti kuwa; “Silali usiku, naangalia video nyingi sana kuona jinsi ninavyoweza kuiboresha Yanga kwa kuusoma uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na kundi lote, kuona jinsi tunavyoweza kucheza soka nzuri.”

“Nashukuru viongozi wamefanya usajili mzuri sana na siyo kusema kwamba hakuna sehemu ya kurekebisha lakini timu hii ni nzuri sana. Hata ukiangalia mechi na Coastal ni watatu tu walicheza ambao walikuwa msimu uliopita, hapo maana yake ni kwamba asilimia 80 ya timu ni mpya na muda unakwenda. Tunahitaji kushinda na kuijenga timu.”

“Nataka timu yangu imiliki mpira, icheze mpira, itengeneze nafasi. Kama tunacheza na timu inayojilinda nataka tucheze, tuwalazimishe wacheze. Nataka timu yangu itawale uwanja, nataka wakati tunacheza timu yangu iwe mbali na goli langu tushinde kwenye upande wa mpinzani, tukae kwenye goli lao,” aliongeza Kaze ambaye amewahi kuzifundisha timu za vijana na ile ya wakubwa ya Burundi kwa nyakati tofauti pamoja na kuwa kwenye akademi ya Barcelona ya Hispania.