Kaze: Nilihusika usajili wa wachezaji hawa Yanga

KWA mara ya kwanza, Kocha wa Yanga, Mrundi Cedrick Kaze amezungumza na Mwanaspoti na kuthibitisha alihusika kwenye usajili wa mastaa wapya wa kigeni wa klabu hiyo.

Lakini amesisitiza ubingwa wa msimu huu utaamuliwa kwa tofauti ya pointi na mabao huku akisisitiza anajua cha kufanya kukamilisha kiu ya mashabiki wa Yanga.

Kocha huyo amethibitisha atatua alhamisi saa 4 usiku kwa ndege ya KLM. “Ni kweli nimefuatilia kikosi chote tangu ligi inaanza na wachezaji karibu wote haswa hawa wa kigeni nimewafuatilia kwa karibu.

Wakina Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Yacouba Sogne na Sarpong ni wachezaji ambao walikuwa kwenye chaguo langu. Mchezaji ambae sikuwa namjua vizuri ni Carlinhos, lakini tangu ligi imeanza nimeangalia ni mchezaji mzuri kwenye kupiga faulo, anajua kutoa pasi nzuri, frikiki anazimudu, kwenye boksi ni mtu hatari sana. Nimemkubali,” alisema Kaze kwa njia ya simu.

“Wachezaji wengine wazawa kama kina Bakary (Mwanyeto), Metacha (Mnata), Yasin (Mustapha), Kaseke (Deus), Feitoto, Mauya, Ditram (Nchimbi ni wachezaji wazuri wameonyesha kiwango kizuri, wana kitu kizuri ambacho ninaweza kukitumia kuifanya Yanga icheze vizuri na kwa mafanikio.

“Nimeangalia mechi zote za ligi tangu ile ya Tnzania Prisons hadi hii ya mwisho ya Coastal Union tuliposhinda mabao 3-0, nimeangalia pia na mechi za timu zingine ikiwemo Simba, Azam, Namungo, Polisi na timu karibu zote. Nimewaangalia kupitia Azam, nimeona levo yetu na wapinzani wetu, nimeona viwanja vya Dar es Salaam na mikoani sasa naweza kusema nina picha halisi ya kila kitu ninachokuja kufanya, nimeshuhudia hadi mechi za kirafiki, nakuja kuanza kazi sehemu ambapo najua kila kitu.

“Nimeona mambo mengi kwenye timu yangu lakini ligi ni ngumu. Upinzani ni mkubwa sana, bingwa atapatikana kwa tofauti ndogo sana, ligi itakuwa na upinzani mkubwa mpaka mwisho. Kila mchezo tunaocheza unapaswa kuwa kama fainali yetu, najua hii ligi tofauti ya pointi itakuwa ndogo sana, kila kitu kitakuwa sawa kwa hizi timu za juu hakutakuwa na mambo ya ugenini wala nyumbani.