JICHO LA MWEWE: Kauli ya Nahimana kwa Simba inafungua sura mpya

Tuesday June 2 2020

 

By EDO KUMWEMBE

HATUISHIWI vituko. Labda usafiri kwenda nchi nyingine lakini hapa nchini huwa hatuishiwi. Majuzi kipa wa KMC, Jonathan Nahimana amelazimika kuiomba radhi klabu yake baada ya kutangaza hadharani hamu yake ya kuichezea Simba.

Mwandishi mmoja wa Wasafi Radio aliyepo Burundi aliongea naye, kipa akajaa katika anga zake na kutangaza kwamba anatamani kuichezea Simba. Klabu yake iliyo chini ya Meya wa jiji la Kinondoni, Benjamin Sitta imekuja juu na kumsimamisha.

Kuna maswali ya kujadili. Mara nyingi wachezaji wa timu ndogo huwa wanaeleza tamaa zao wa kucheza katika klabu kubwa. Kwa wenzetu hali inakuwa tofauti kidogo. Kwa mchezaji wa timu kubwa kama vile Tottenham hawezi kutangaza nia yake ya kutamani Manchester United.

Hata kama anatamani atakaa kimya. Kwa Ligi yetu, KMC ni kama Tottenham pale England. Sio timu kubwa lakini sio timu ndogo. Kutamani hadharani ni kuidhalilisha klabu yako. Alipaswa kutunza heshima kidogo.

Mara nyingi wachezaji wanaocheza England, wawe raia au sio raia wa England, muda wowote wanaweza kuelezea matumaini yao ya kucheza katika klabu kubwa za Hispania, Italia au Ujerumani. Hawawezi kuelezea nia yao ya kucheza katika klabu kubwa za ndani.

Kwa mfano, Harry Kane ukimuuliza kama angependa kucheza Real Madrid au Barcelona anaweza kuwa wazi. Hata hivyo, hawawezi kuweka wazi kwamba anatamani kucheza Manchester United au Chelsea. Hawa ni wapinzani wake wa pale pale England.

Advertisement

Inaweza kutokea siku moja atajikuta akicheza Manchester United. Siku ile ile ya kukabidhiwa jezi akaelezea namna alivyokuwa na hamu ya kujiunga na klabu hiyo. Utamsikia tu akisema “Imekuwa ndoto yangu kuichezea Manchester United tangu nikiwa mdogo. Nashukuru kwamba lengo langu leo limetimia. Shukrani kwa timu yangu ya zamani Tottenham ambayo imeniwezesha kufika hapa”.

Huyu ndiye mchezaji aliyeiva hasa. Ni ngumu kwake kusema hivi akiwa bado hajasaini Man United. Kwa wakati huo akiwa mchezaji wa Tottenham atajikita zaidi katika kuelezea namna ambavyo ana furaha na timu yake.

Hapo hapo ni vema kukumbuka kwamba upinzani kati ya Manchester United na Tottenham upo karibu zaidi. Ni kama ambavyo ilivyo hapa, licha ya Simba kuwa timu kubwa zaidi ya KMC lakini ni wazi KMC wana upinzani mkubwa kwao kuliko ilivyo Ndanda.

Lakini hapo hapo kuna jambo jingine linajitokeza. Huyu kipa wa KMC amebakiza mwezi mmoja tu katika mkataba wake. Ni rahisi kwake kusaini mkataba wa awali na klabu yoyote anayoitaka kwa sasa. Kwa England unaruhusiwa kufanya hivyo kwa klabu ya nje ya England. Ni kama vile Aaron Ramsey alivyosaini mkataba wa awali na Juventus angali akiwa na Arsenal.

Sijui kanuni zetu zinasemaje kuhusu suala la kusaini mkataba wa awali miezi sita kabla, lakini hapo hapo tujiulize, inakuwaje kwa mchezaji ambaye hajasaini mkataba na anatamani? Na ni vipi kama anaitamani klabu ya ndani ya Ligi?

Pale Ujerumani nadhani inaruhusiwa kusaini mkataba wa awali na klabu nyingine ya ndani. Kwa mfano, Mario Gotze na Robert Lewandowski katika nyakati tofauti walisaini mikataba ya kuichezea Bayern Munich miezi sita kabla ya kuhama.

Lewandowski alifanya hivyo Januari. Alizomewa vilivyo na mashabiki wa Borussia Dortmund lakini hii ndio ilikuwa hali halisi. Baadhi ya mabosi wa Dortmund walikasirishwa na hali hii hasa ukizingatia kwamba alikuwa anakwenda kwa wapinzani wao wakubwa katika Ligi lakini haikusaidia.

Hapa najiuliza. Nahimana amesema tu anatamani kuichezea Simba. Inawezekana hili ni kosa kuliko kama angetangaza kusaini mkataba wa awali na Simba na kuweka hadharani. Labda lisingekuwa kosa. Au sheria zetu ni tofauti na zile za nje?

Inawezekana nasi tunafuata nyayo za Waingereza kwamba labda angeelezea hisia zake za kutamani kuchezea TP Mazembe huenda lisingeonekana tatizo miongoni mwa mabosi wa KMC. Labda ingekuwa poa tu.

Mwisho wa siku tunahitaji ufafanuzi katika suala hili la Nihimana. Tanzania mchezaji anaweza kusaini mkataba wa awali (Pre contract) miezi sita kabla kwa timu nyingine ambayo ipo ndani ya Ligi. Vipi suala la kuizungumzia?

Na tukirudi katika suala la kuizungumzia Simba tu, KMC wenyewe wanajikuta katika wakati mgumu kwani mchezaji mwenyewe amebakiza mwezi mmoja tu kuwa mali yao kwa mujibu wa mkataba wake.

Ni adhabu gani wanayoweza kumpa katika mwezi huu. Nadhani hawawezi kumfungia kucheza soka kwa zaidi ya muda ulio nje ya mkataba wake. Watalazimika kunywea zaidi hasa kama wanamhitaji kipa huyo.

Pamoja na yote haya nadhani tunarudi kule kule tu. Wachezaji wetu wanahitaji umakini wanapoongea na vyombo vya habari. Wengi wao wanaongea bila ya weledi na kusababisha utata usio wa lazima.

Advertisement