Katibu Mkuu Yanga bado kizungumkuti

Muktasari:

Chanzo cha ndani ya Yanga kimeongeza Kamati inayoratibu mchakato wa kupatikana kwa katibu imeshindwa kupata anayekidhi, hivyo watatoa tangazo jipya la kuomba kwa nafasi hiyo likiwa limefanyiwa marekebisho tofauti na lile la awali na hasa suala la elimu.

KAMA wanachama wa Yanga walikuwa wakijiandaa kumjua Katibu Mkuu wao mpya, basi waendelee kusubiri tu, kwani mchakato huo uliokuwa umefikia patamu na kupatikana kwa majina mawili yakipewa nafasi ya kutangazwa, sasa unaanza upyaaa!

Awali Mwanaspoti lilipenyezewa taarifa aliyekuwa Mtendaji Mkuu Azam, Saad Kawemba na meneja wa zamani klabu hiyo ya Chamazi, Jemedari Said ndio walikuwa wamepenya sambamba na mtu mmoja wa benki ambaye hata hivyo alitemwa.

Kawemba na Jemedari mmoja wao ndiye aliyekuwa atangazwe kushinda nafasi hiyo, lakini ghafla mabosi wa klabu hiyo wakagawanyika, wengi wakiona Kawemba anayestahili kwa vigezo, huku kigogo mmoja akimtaka Jemedari na kufanya mchakatio uanze upya. Nafasi hiyo ipo wazi tangu alipojiuzulu Boniface Mkwasa ambaye nafasi yake ilikaimiwa na Omar Kaya aliyemaliza muda na kuachwa kwa sasa kwa Dismas Ten na ambaye naye mkataba wake Jangwani ulishamalizika na alitakiwa kukabidhi kwa katibu Mpya ajaye.

Chanzo cha ndani ya Yanga kimeongeza Kamati inayoratibu mchakato wa kupatikana kwa katibu imeshindwa kupata anayekidhi, hivyo watatoa tangazo jipya la kuomba kwa nafasi hiyo likiwa limefanyiwa marekebisho tofauti na lile la awali na hasa suala la elimu.

Sifa ya awali ya elimu ililenga mwenye elimu ya Shahada ya Chuo Kikuu, lakini viongozi waliojitokeza wamekosa sifa na sasa wanataka kushusha iwe Stashahada na uzoefu wa masuala ya soka kwa muda mrefu.

“Mchakato utakaofanyika ni wanafasi ya Katibu Mkuu pekee, lakini kwa zile nyingine za Sekretarieti tayari zimeshapata viongozi wa kuziongoza na muda wowote kuanzia leo watatangazwa,” kilisema chanzo hicho.

Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla alipotafutwa na Mwanaspoti ili kufafanua juu ya jambo ilo alisema ni masuala ya ndani ya klabu yao, hivyo hawezi kulizungumzia hadi mambo yatakapokamilika.

“Kuna kamati inaratibu suala hilo, hivyo sio wakati muafaka kulizungumzia sasa mchakato bado unaendelea na wengi wamejitokeza kuomba nafasi hiyo, muda ukifika tutalizungumzia,” alisema Dk Msolla aliyechaguliwa kwenye nafasi hiyo Mei mwaka huu.