Pamba yasimamisha Jiji, yapokelewa kishujaa Mwanza

Muktasari:

  • Pamba ambayo imepanda daraja Jumapili iliyopita jijini Arusha baada ya kuichapa Mbuni FC mabao 3-1 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kumaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi 67 nyuma ya vinara, Ken Gold

Mwanza. USIPIME! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mapokezi makubwa iliyoyapata Pamba Jiji leo baada ya kupanda daraja kwenda Ligi Kuu Bara mwishoni mwa wiki iliyopita ikivunja mwiko wa miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001.

Msafara wa timu hiyo uliokuwa umebeba wachezaji, benchi la ufundi na baadhi ya viongozi uliokuwa unatokea Arusha kupitia mkoani Shinyanga umepokelewa leo saa 4:30 asubuhi katika mji mdogo wa Hungumalwa wilayani Kwimba, Mwanza na kuanza safari ya kuzunguka Jiji la Mwanza ikipita vituo mbalimbali vya mapokezi.

Msafara huo ambao umelakiwa na kusindikizwa kwa mbwembwe na madereva pikipiki (bodaboda) na bajaji umepita Misungwi, Buhongwa, Mjini Kati, Buzuruga, Nyasaka, Pasiansi na kuishia Uwanja wa Nyamagana ambapo viongozi mbalimbali na wakazi wa jijini hapa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Said Mtanda wamezungumza na kutoa pongezi kwa wachezaji na benchi la ufundi.

Katika maandamano hayo kupitia maeneo mbalimbali kwenye Barabara ya Nyerere na Kenyatta shughuli mbalimbali za kijamii zilisimama wananchi wakisimama barabarani kuwapungia mkono wachezaji na benchi la ufundi waliokuwa kwenye gari kubwa la wazi.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mapokezi hayo kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewashukuru mashabiki kwa kuwa na timu wakati wote huku akiwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na menejimenti kwa ushirikiano uliowezesha timu hiyo kupanda daraja.

"Manufaa baada ya Pamba kupanda daraja ni kuongeza mapato ya jiji kupitia ushuru wa huduma na viingilio uwanjani, kukuza vipaji vya soka kwenye mkoa wetu, kuongeza ajira na tunataka kuifanya Mwanza kuwa Jiji la utalii wa michezo," amesema Mtanda.

Mtanda amesema baada ya kufanikisha kuipandisha daraja Pamba Jiji, nguvu zake anazihamishia kwa Biashara United ili kuhakikisha nayo inapanda daraja kwa kushinda mechi zake za mtoano.

"Mimi na Amos Makalla tuliahidi tuipandishe kwanza Pamba halafu tutaisaidia Biashara United kwa sababu hii ni Kanda ya Ziwa. Kwa hiyo tumejipanga kuisaidia Mara kuipandisha Biashara United ipande. Na Mimi nitatoa nguvu zote kuhakikisha Biashara United wanaishi vizuri na wanapata wanachoihitaji ili wakishindwa washindwe kwa sababu zingine."

"Lazima tuwasaidie Biashara United kwani tunataka Kanda ya Ziwa turudishe nguvu na uwezo wetu," amesema Mtanda ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na mlezi wa Biashara United kabla ya kuhamishiwa Mwanza zikiwa zimebaki mechi tatu kumaliza Ligi ya Championship.

Mdau wa soka jijini hapa, Jamal Babu amesema kuipandisha daraja Pamba Jiji halikuwa jambo dogo ambapo wametoa ushirikiano muda wote kuhakikisha Mwanza inapata timu ya Ligi Kuu.

"Tuna kila sababu kama Mkoa kumpongeza Amos Makalla kwa kuwaita wadau na kuipandisha Pamba Jiji japo mwanzo ilikuwa ngumu lakini leo tunaona matunda yake. Natoa salamu za pongezi kutokana na juhudi ambazo zimefanyika na tunawatia nguvu na morali wakati tukielekea kwenye ligi kwa sababu bado wadau hawa wanahitajika, tuhakikishe tunaweka nguvu ya kiuchumi ili kuhakikisha Pamba inafanya vizuri Ligi Kuu," amesema Babu.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Vedastus Lufano amesema mashabiki wa soka mkoani humo wanapaswa kuwa na imani kwani timu hiyo iko mikono salama huku akiahidi kutoa ushirikiano katika maandalizi ya Ligi Kuu.

Nahodha wa timu hiyo, Jerry Tegete, amesema mapokezi makubwa waliyoyapata wanastahili kwa namna ambavyo wameipambania timu hiyo, huku akiwaomba mashabiki na wadau kuendelea kuwaunga mkono katika safari yao mpya ya Ligi Kuu.