Kashfa ya Mwendwa alivyobeba Joy Riders AFCON 2019

Tuesday November 12 2019

Kashfa - Mwendwa -alivyobeba- Joy -Riders- AFCON- 2019-RAIS - Shirikisho - soka-kenya

 

By Thomas Matiko

Nairobi, Kenya. RAIS wa Shirikisho la soka nchini FKF, Nick Mwendwa yupo bize akipambana na hali yake kujitetea kuhusu sakata la ubadhirifu wa Sh244 milioni zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ushiriki wa dimba la AFCON.

Siku za hivi karibuni Mwendwa amekuwa kwenye malumbano makali na Katibu wa Kudumu katika Wizara ya Michezo Peter Kaberia. Mwendwa amemshtumu kaberia kwa kugoma kutoa hela za kuifadhili timu za taifa Harambee Stars na ya kinadada Harambee Stars kwenye majukumu yao yajayo ya kitaifa.

Hata hivyo, Kaberia naye alimpasha Mwendwa akimtaja ni mtu asiye na shukrani na aliyekosa uaminifu baada ya kushindwa kuwajibika jinsi alivyotumia Sh244 milioni.

Sasa uchunguzi uliofanywa na wanahabari wa Kimichezo wa Nation umegundua Mwendwa alifuja sehemu kubwa ya fedha hizo akitumia mita kadhaa kuwasafirisha watu wasiohusika ‘joy riders’ kwenda Cairo, Misri wakiongozana na Harambee Stars.

Wanasema msafara wa mamba haukosi mburukenge na hakika ndicho alichokifanya Mwendwa akiishia kutumia mamilioni ya pesa za watoza ushuru kugharimia safari ya watu wake ambao hawakuwa wahusika kabisa katika masuala ya timu ya taifa kwenye ushiriki wake AFCON.

Kulingana na stakabadhi tulizozinasa zinaonyesha Mwendwa ndiye aliyepokea marupurupu ya kiwango cha juu zaidi kwa kipindi chote Stars ilikuwa kule Misri kwa mtanange huo uliopigwa kati ya Juni 21 hadi Julai 19 Senegal wakitwaa ubingwa.

Advertisement

Stakabadhi hizo zinaonyesha Mwendwa alilipwa marupurupu ya Sh50,000 kwa kila siku aliyokuwa kule Misri.

Kiasi hiki kilikuwa kikubwa hata zaidi ya maofisa wakuu wa serikali walioongozana na timu hiyo pia kuishabikia na kuwapa morali.

Hata hivyo, Mwendwa hakuwa mwenyewe. Alisafiri na naibu wake Doris Petra aliyepokea marupurupu ya Sh45, 000 kila siku. Kisha wanachama nane wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya Shirikisho hilo kila mmoja akilambishwa Sh40, 000 kwa siku.  Ofisa Mkuu Mtendaji wa FKF aliyefutwa kazi wiki kadhaa zimepita Robert Muthomi naye alipokea Sh35,000 kila siku.

Kisha kulikuwa na wasaidizi wa Shirikisho waliolipwa Sh10,000 kwa kila siku waliyokuwa kule na mabosi wao hao. Hao ni kama vile msaidizi wa kibinfasi wa Mwendwa Sylivia Mumbua, msaidizi wa kibinfasi wa Muthomi, Julie Nyambura, Hasibu mkuu wa FKF Christine Ojode miongoni mwa wengine

Ushiriki wa Stars Cairo hadi walipopanduliwa ulidumu kwa siku 13, muda ambao Mwendwa na kikosi chake kilikuwa kikikamua tu hela.

Kwa hesabu za haraka, FKF ilitumia zaidi ya Sh5 milioni kati ya zile Sh244 milioni kuifurahisha timu yake ambayo haikuhitaji kabisa kusafiri na Stars.

Hata hivyo, FKF wamejitetea dhidi ya matumizi hayo kwa kusema ilikuwa ni wajibu wao kujali masilahi ya wanachama wake.

“Ni utaratibu wa shirikisho kugharimia malazi ya wanachama wake wa matawi wenye uwezo wa kugharimia nauli zao kwa ajili ya dimba kubwa. Kamati Kuu ya FKF lazima ingesafiri na timu hasa ikizingatiwa Kenya ilikuwa inarejea katika mashindano haya baada ya kuikosa kwa miaka 15,” alisema Barry Otieno ambaye kajaza mahala pake Muthomi kama CEO wa shirikisho.

Mapema Jumatatu Mwendwa aliraukia hadi kwenye kituo cha radio cha Hot 96 kujitetea  dhidi ya ubadhirifu huu ambao umekuwa ukianikwa na timu ya Nation.

“Wanasema niliwapeleka joy riders AFCON. Huo  ni uwongo mtupu. Tuliwasafirisha pia waandalizi video kutengeneza matukio ya timu yetu kule ili kuvitumia vyombo vya habari hapa nchini kwa sababu hakuna shirika la habari lililotupa wanahabari wake Misri kuangazia ushiriki wetu.”

Kauli ya Mwendwa ni uwongo mtupu hasa ikizingatiwa kampuni ya Nation Media Group liliwatuma wanahabari wawili kwenda Misri kuangazia michuano hiyo. James Otwal wa runinga ya NTV na Charles Nyende wa  gazeti la Daily Nation wote walikuwa Misri.

Vile vile kituo cha runinga ya K24 pia kilimtuma mwanahabari wake Shawn Osimbo.

Advertisement