Karia awajaza upepo wadau

Sunday August 2 2020

 

By MUSSA MWANGOKA, SUMBAWANGA

MKOA wa Rukwa kwa muda mrefu sasa hauna timu ya Ligi Kuu tangu klabu za Ujenzi Rukwa na Katavi kushuka daraja, lakini Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia amewajaza upepo wadau wa soka mkoani hapa, wakitaka wakazane ili kurejea kwenye ramani ya soka kama zamani.

Karia aliyasema hayo juzi wakati wakizungumzia maandalizi ya mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga kati ya Simba na Namungo.

Rais huyo wa TFF, alisema baada ya fainali hiyo ni wakati wa wadau wa soka mkoani Rukwa, ikiwemo viongozi wa wa vyama vya soka na serikali kutafakari kwanini mkoa huo wenye uwanja mzuri unakosa timu ya kushiriki madaraja ya juu ikiwemo Ligi Kuu kisha kujipanga kufuta unyonge huo.

“Tumeleta fainali hii, huku Rukwa ili kukufua Uwanja wa Nelson Mandela ambao ulikuwa haupo katika ubora kutokana na kutofanyiwa marekebisho ya mara kwa mara, pia kuleta chachu ya kuhakikisha wadau wa soka wanaona umuhimu wa kupata timu ya ligi kuu,” alisema Karia

Pia Karia, alisema kukarabatiwa kwa uwanja wa Nelson Mandela kutafungua fursa ya timu kutoka mikoa ya jirani kama Mbeya, Katavi na Kigoma pia nchi jirani za Kongo DRC, Zambia na Burundi kucheza michezo ya ujirani mwema hivyo kuleta hamasa ya kuinua soka mkoani humo.

Advertisement