Kama utani tu wametema kitambaa

Muktasari:

  • Wapo manahodha wengi ambao kwa namna moja au nyingine iliwabidi kuwapisha wenzao kwa sababu mbalimbali.

MANAHODHA ni viongozi wa wachezaji uwanjani. Ndio wanaohakikisha nidhamu kwa wachezaji wenzao, pia ndiye anayewasiliana na mwamuzi wakati wa tukio lolote la kiuchezaji.

Manahodha huteuliwa na kocha na huwa na wasaidizi endapo atapata dharura yoyote iwe ni kuumia au kutokuwepo kwenye mchezo husika. Hata hivyo, endapo atakiuka maadili ya kukitumikia kitambaa cha unahodha ambacho ni hadhi kubwa kwake, ni rahisi kwa kocha kuamua kumtema na kumteua mwingine mwenye sifa zinazostahili.

Wapo manahodha wengi ambao kwa namna moja au nyingine iliwabidi kuwapisha wenzao kwa sababu mbalimbali.

AGGREY MORRIS

Tangu Azam FC ipande daraja kushiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2007/08, amekuwa nahodha wake kabla ya mambo kutibuka msimu wa 2012/13 alipokuwa na matatizo na uongozi wa klabu hiyo.

Matatizo hayo yalisababisha kukaa nje ya uwanja kwa muda na hivyo, nafasi yake kukaimu John Bocco akikivaa vyema kitambaa cha unahodha na kuisaidia Azam kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013/14. Bocco alidumu na kitambaa hicho hadi alipoachana na timu hiyo na kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Simba.

Hata hivyo, kwa sasa ndiye nahodha wa timu hiyo na wili iliyopita aliisaidia Azam kutwaa taji la Mapinduzi wakiifunga Simba mabao 2-1 kwenye michuano hiyo iliyofanyika visiwani Zanzibar.

JONAS MKUDE

Benchi la ufundi la Simba, chini ya Kocha wake mkuu, Joseph Omog liliamua kufanya marekebisho kwenye nafasi hiyo nyeti uwanjani ya unahodha baada ya kumvua kitambaa cha unahodha Mkude na kumpa beki wa kimataifa Mzimbabwe Method Mwanjali.

Hata hivyo, Mwanjali hakuitumikia kwa muda mrefu nafasi hiyo baada ya kuondoka Simba huku Mkude akiendelea kuwa mchezaji mwandamizi kwenye klabu hiyo na kuishia kukiona kitambaa hicho cha unahodha kwa wenzake.

Aliyerithi kitambaa cha Mwanjali alikuwa ni Mohammed Hussein (Tshabalala) na kwa sasa nahodha ni John Bocco ambaye ameiongoza Simba tangu ajiunge nayo akitokea Azam FC alikokuwa pia nohodha na ameisaidia Simba kutwaa taji la Ligi Kuu Bara na sasa ikifanya vyema kwenye mehi za kimataifa ikifuzu hatua ya makundi.

KELVIN YONDANI

Ndiye mwamba wa Yanga akikitumikia kitambaa cha unahodha tangu aliyekuwa nahodha wake Nadir Haroub Cannavaro aliyestaafu soka. Ilikuwa kama utani

baada ya Zahera kuamua kumvua kitambaa cha unahodha na kumpa Ibrahim Ajib kutokana na Yondani kushindwa kufika mazoezini bila kutoa sababu.

Januari 4, mwaka huu Zahera ndio alifanya uamuzi huo na kuzua mijadala mingi kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, huku wapenzi wa soka wakihoji msimamo wa kocha japo hawakuweza kuubadilisha baada ya kuweka wazi anaendesha mpira kwa kusimamia nidhamu michezoni na kusisitiza mchezaji asiye na nidhamu hana nafasi kwenye kikosi chake.

NADIR HAROUB ‘CANNAVARO’

Ulikuwa ukiitaja Taifa Stars, jina la kwanza kukujia kichwani linaweza likawa la Cannavaro. Aliwaongoza nyota wenzake wa Stars kwa miaka mitano kabla ya kuja kuvuliwa na aliyekuwa Kocha wa Stars Charles Boniface Mkwasa na kumkabidhi nahodha wa sasa wa Stars Mbwana Samatta anayekipiga soka la kulipwa kwenye klabu ya Genk ya Ubelgiji.

Samatta alikabidhiwa kitambaa hicho kama heshima baada ya kutoka kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani.

Cannavaro ambaye alikuwa ni nahodha wa klabu yake ya Yanga na Zanzibar Heroes baada ya kuvuliwa kitambaa hicho aliamua kustaafu kuichezea Stars, huku Mkwasa akitetea uamuzi wake wa uteuzi wa Samatta ni wa kawaida.

Mara ya mwisho Cannavaro aliiongoza Stars akiwa nahodha baada ya kufungwa mabao 7-0 na Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

HASSAN ISIHAKA

Kitendo cha Isihaka kumtolea majibu yasiyostahili kocha wake Jackson Mayanja kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida United Februari 28 mwaka 2016.

Kamati ya Utendaji ya klabu ya Simba ilisema kutokana na ukubwa wa klabu ya hiyo na uzito wa kosa alilolifanya waliamua kumvua kitambaa hicho.

Inadaiwa Isihaka hakupendezwa na kitendo cha kocha huyo kumweka benchi katika mechi kadhaa hususan dhidi ya Yanga kisha kumpanga kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Singida United.