Kakolanya ashtukia mtego Jangwani

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Richard alisema Yanga imefanya kitu ambacho sicho walichokihitaji, hivyo ameamua kumuomba Kaya waweze kukutana na kuzungumza mambo mengi kuhusiana na Kakolanya ikiwamo pesa waliyoingiza katika akaunti.

UKISIKIA kutegeana ndiko huku, wakati mabosi wa Yanga ukimuingizia pesa ya mshahara katika akaunti yake, kipa Beno Kakolanya kupitia Mwanasheria wake Leonard Richard ameomba kukutana na uongozi wa klabu hiyo ili kumalizana.

Mwanasheria huyo alisema wanataka kukutana na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya ili afafanue masuala mbalimbali ikiwa pamoja na fedha hizo wanazomwekea mteja wake sambamba na kusikilizia juu ya ombi lao la kutaka avunjiwe mkataa ambao muda wake uliisha tangu Januari 12.

Akizungumza na Mwanaspoti, Richard alisema Yanga imefanya kitu ambacho sicho walichokihitaji, hivyo ameamua kumuomba Kaya waweze kukutana na kuzungumza mambo mengi kuhusiana na Kakolanya ikiwamo pesa waliyoingiza katika akaunti.

Alisema ameiandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Yanga kuiomba Kakolanya aachwe baada ya kukiuka baadhi ya vipengele katika mkataba wake, lakini hakuna jibu hadi sasa zaidi ya kufahamishwa na kipa huyo anaingiziwa fedha.

“Bado hatujapata majibu kutoka sehemu yoyote lakini sasa nilichukua jukumu la kumpigia simu Kaya ambaye hakuipokea nikamtumia ujumbe mfupi wa maandishi kumuomba muda wake ili niweze kukaa naye pamoja na kujadili suala la barua ikiwa pamoja na suala la wao kumuingizia fedha,” alisema.

“Nimepewa taarifa na mteja wangu kwamba kuna pesa kaingiziwa lakini bado sijajua ni kwa ajili ya nini kwani ni muda sasa yupo nje ya timu, tunachotaka wamruhusu kwani kuna timu ya nje inamtaka.”

Mwanasheria huyo alisema atakuwa na mengi ya kuzungumza na Kaya ili aweze kumpa ufafanuzi zaidi ya mambo kuhusu mteja wake na ajulishwe kwanini hajapewa majibu yake baada ya kuwakabidhi barua kabla hajafuata hatua nyingine.

Sakata la Kakolanya lilianza baada ya kugoma kujiunga na timu hiyo akidai kupewa pesa zake za usajili, mara nyingi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera akisema hataki tena kumuona kikosini mlinda mlango huyo kutokana na kujiondoa mwenyewe.

Licha ya kocha huyo kuonyesha hamtaki kipa wake ndani ya kikosi hiko, Yanga imekuwa ikijivuta kwenye maamuzi ya kuachana na Kakolanya kiasi cha kumfanya mchezaji huyo kuandika barua ya kutaka avunjiwe mkataba ili atafute maisha mengine nje ya Jangwani.

Mapema Meneja wa Kakolanya, Seleman Haroub aliamua kufuata sheria kwa kuwatafuta Wanasheria ili kumfanya mchezaji wake awe huru lakini mpaka sasa hakuna ufumbuzi wowote uliopatikana.