Kagere, Dilunga na Mkude waacha msala Mwanza

Tuesday January 21 2020

Kagere, Dilunga na Mkude waacha msala Mwanza-Uwanja wa CCM Kirumba-Mbao vs Alliance-,Simba SC-Smba Sports Club-Msimbazi-

 

By Saddam Sadick,Mwanza

SIMBA juzi ilikamilisha wiki kwa kishindo kutokana na ushindi mfululizo katika Uwanja wa CCM Kirumba kwa kuzichapa Mbao na Alliance, huku muziki wa nyota wake ukiacha gumzo.

Timu hiyo ambayo inaongoza Ligi Kuu kwa pointi 41, ilifanya balaa kwa kutembeza vichapo kwa wapinzani wao ikianza na Mbao iliyowalaza mabao 2-1 kisha kuishindilia Alliance 4-1.

Katika mechi hizo, Simba ilionyesha kiwango bora isipokuwa hali ya uwanja haukuwa rafiki kutokana na mvua iliyokuwa imenyesha na kusababisha kukosa burudani kwa timu hizo.

Mwanaspoti ambayo ilifuatilia mechi zote za timu hiyo, inakuletea jinsi Wekundu hao walivyoacha msala jijini hapa na mwelekeo wa vinara hao kwenye Ligi Kuu.

Ushindani

Katika michezo miwili iliyocheza Simba katika Uwanja wa Kirumba, Simba ilionyesha ushindani mkali na kuonekana kuwazidi wapinzani jambo ambalo liliwapa ushindi.

Advertisement

Licha ya Mbao na Alliance kujaribu kupambana, lakini kiuhalisia Wekundu hao walikuwa bora katika idara zote, huku mashabiki nao wakiongeza kitu kwa mabingwa hao watetezi.

Katika mchezo wa kwanza ulioikutanisha na Mbao, Simba ndio ilitangulia kupata mabao mawili, la kwanza katika dakika ya 41 kupitia kwa Hassan Dilunga kisha Jonas Mkude kuiongezea la pili katika dakika ya 46.

Licha ya Mbao kulazimisha mashambulizi na kufanikiwa kujipatia bao la kujifariji kupitia kwa Waziri Junior katika dakika ya 52, lakini kwa asilimia kubwa Simba iliutawala mchezo.

Katika mchezo na Alliance, licha ya Simba kutanguliwa bao katika dakika ya 27 kupitia kwa Israel Patrick, lakini vigogo hao wa Ligi Kuu walikuwa moto muda wote na kuweza kusawazisha bao hilo kabla ya kwenda mapumziko kupitia kwa Mkude.

Nguvu ya mashabiki

Pamoja upambanaji ndani ya uwanjani kwa wachezaji wenyewe, lakini nguvu ya mashabiki wa Simba iliwaongezea morali timu kwani walicheza kama wako nyumbani.

Tangu kuwasili kwa Simba Jijini hapa, ilishuhudiwa mashabiki wakijitokeza kwa wingi kuanzia kwenye mazoezi hadi siku za mechi, jambo ambalo lilikuwa likiwapa hamasa wachezaji.

Timu za Mbao na Alliance licha ya kwamba zilikuwa nyumbani, lakini nguvu kwa mashabiki wao ilikuwa ndogo kulinganisha na wapinzani wao hivyo kuweka utofauti pande zote.

Katika michezo yote, mashabiki wa Simba walijitokeza kwa wingi na muda wote walikuwa wakiishangilia timu yao pale walipoona wachezaji wakifanya vizuri.

Kagere, Mkude na Dilunga

Miongoni mwa wachezaji walioacha gumzo jijini Mwanza ni wachezaji watatu wa Simba kutokana na kasi yao iliyowaacha hoi mashabiki wa timu hiyo wakibaki midomo wazi.

Straika wa kimataifa wa Rwanda, Kagere ambaye alikuwa hajafunga bao tangu Jan 4 alipoifunga Yanga, aliwajibu waliokuwa wanambeza kwa kutupia bao dakika ya 59.

Kagere ambaye alifikisha bao lake la 11 na kuwaacha wapinzani wake, Paul Nonga (8) na Daruweshi Saliboko mwenye saba, alifunga bao hilo kwa kichwa akimalizia mpira wa Sharaf Shiboub na kuamsha shangwe.

Nyota huyo ambaye anatetea kiatu chake cha mfungaji bora, alikosa mchezo uliopita dhidi ya Alliance FC kutokana adhabu aliyokuwa nayo ya kutumikia kadi tatu za njano.

Ukiachana na Kagere, sura nyingine iliyoacha msala Mwanza ni kiungo wa ulinzi, Jonas Mkude ambaye aling’ara kwa mechi mbili mfululizo kwa kutupia mabao muhimu.

Mkude ambaye alikuwa hajafunga bao lolote katika mechi alizokuwa amecheza katika Ligi Kuu msimu huu, aling’ara kwenye dimba la Kirumba kwa mabao yake mawili ambayo aliyafunga kiufundi zaidi.

Bao la kwanza alilofunga wakati Simba ikiilaza Mbao, aliunganisha vyema mpira wa kona iliyochongwa na Ibrahim Ajibu na kisha kuunganisha vyema mpira wa Shiboub wakati wakiirarua Alliance mabao 4-1.

Nyota mwingine ambaye alikuwa shujaa zaidi katika mechi zote ni Hassan Dilunga ambaye alihusika kwa mafanikio yote ya timu hiyo kwenye jiji la Mwanza na kuiwezesha timu hiyo kuondoka kibabe.

Kasi ya Kiungo huyo na pasi za macho, alikuwa moja ya wachezaji waliofanya kazi ya ziada na kuisaidia Simba kuzoa pointi zote sita kwenye mechi hizo.

Dilunga akicheza katika ubora wake, alifunga mabao mawili kwa kutupia kila mchezo na kubwa zaidi ni ufungaji wake mabao matamu sana likiwamo la shuti la roketi la kutokea nje ya 18.

Mbelgiji anogewa

Baada ya dakika 180 kumalizika uwanjani hapo, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck hakusita kuwapongeza vijana wake kwa kazi nzuri waliyofanya huku akiweka wazi mikakati ya timu hiyo.

“Mechi ya leo (juzi) tulifanya makosa kipindi cha kwanza, lakini tulirudi na kurekebisha mapungufu na kuweza kupata ushindi lakini bado kazi ni ngumu kuhakikisha tunashinda kila mchezo ili kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema kocha huyo.

Mbao, Alliance wakubali

Kocha wa Mbao FC, Hemed Morocco aliweka kutokuwa makini kwa nyota wake hasa washambuliaji kuliwagharimu.

“Muda mrefu tumekuwa na tatizo la straika, lakini kwa kipindi cha dirisha dogo tumejaribu kulifanyia kazi, hivyo tunaamini katika mwendelezo wa Ligi tutapata ushindi” anasema Morocco.

Naye Kocha Mkuu wa Alliance FC, Fredy Felix ‘Minziro’ anasema kuwa wanakubali kupoteza mchezo huo kutokana na makosa waliyoyafanya na kwamba Simba ni timu kubwa na yenye wachezaji wazuri.

Advertisement