Kagera wamrudisha Mbaraka Yusuph

Friday August 7 2020

 

By MWANDISHI WETU

STRAIKA wa Azam FC, Mbaraka Yusuph amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea timu yake ya zamani, Kagera Sugar baada ya kumaliza mkataba na waajiri wake wa Chamazi.

Mbaraka amesaini mkataba huo leo Ijumaa Agosti 7, 2020 jijini Dar es Salaam na hivyo atajiunga na kikosi chake chenye Kagera mjini Bukoba.

Azam ilimsajili Mbaraka akitokea Kagera Sugar akiwa mfungaji bora wa timu hiyo akifunga bao 12 na sasa anarejea timu yake ya zamani.

Akiwa Azam FC, Mbaraka hakuwa na msimu mzuri tangu atue hapo ambapo amedumu kwa zaidi ya miaka mitatu kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.

Azam ilimsajili mchezaji huyo ambaye wakati huo pia alikuwa akiwindwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili tangu 2017 ambapo baadaye alikwenda kucheza Namungo kwa mkopo na kurudishwa kikosini baada ya Numungo kupanda Ligi Kuu Bara.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Mbaraka amesema; "Ni kweli narudi nyumbani, nadhani huu ni muda wa kucheza, Azam nimemaliza mkataba hivyo nilikuwa mchezaji huru,"

Advertisement

Mbaraka anakwenda Kagera Sugar ambako yupo Kelvin Sabato na Yusuph Mhilu aliyemaliza msimu akifunga magoli 13 ingawa pia anacheza winga.

Advertisement