Kabwili, Shikhalo wambeba Metacha

Muktasari:

Metacha alijiunga na Yanga kabla ya msimu huu akitokea Mbao FC ambayo ilimnasa kutoka katika kikosi cha Azam FC iliyomuibua kutokwa kwenye kikosi chake cha vijana.


KIPA wa Yanga, Metacha Mnata amefichua kuwa ushindani wa wenzake wawili, Farouk Shikhalo na Ramadhan Kabwili umechangia kwa kiasi kikubwa yeye kufanya vizuri na kuweza kuwa chaguo la kwanza ndani ya timu hiyo.

Metacha alisema kuwa uwepo wa makipa hao umemfanya asibweteke na kuridhika jambo ambalo limekuwa na faida kubwa kwake.

"Kipa kuwa tegemeo na hakuna mshindani, lazima kunakuwepo na namna fulani ya kujiamini na morali fulani ya kazi inapungua.

"Lakini ushindani ukiwa mkali, ukipata nafasi huwezi kuichezea,unakuwa unafikiri wale ambao wapo benchi wanasubiri nafasi ya kucheza,hivyo lazima utajituma kwa bidii,"amesema Metacha.

Mnata amesema anaheshimu uwezo wa makipa wenzake  Farouk Shikhalo na Ramadhan Kabwili,akitaja ndio sababu iliyomfanya ajitume kwa bidii kwa kipindi ambacho walikuwa nyumbani.

Amesema ili kiwango chake kiwe juu, lazima akutane na makipa wenye uwezo wa juu kama waliopo katika timu hiyo, akiamini wanakuwa wanampa changamoto ya kujituma..