KUTI KAVU: Valverde inakula kwake Barcelona

BARCELONA, HISPANIA

KISEMWACHO ni hiki, Kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde muda wowote anaweza kufungashiwa virago vyake na kuonyeshwa mlango ulioandikwa ‘exit’ huko Nou Camp kufuatia kichapo cha dharau ilichokipata timu hiyo kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutoka kwa Liverpool na kutupwa nje ya michuano hiyo Jumanne iliyopita.

Barca ilishaichapa Liverpool 3-0 uwanjani Nou Camp kwenye mechi ya kwanza, lakini ilikwenda kukubali kipigo cha 4-0 huko Anfield, licha ya Liverpool ilikosa huduma za mastaa wake kibao wa kikosi cha kwanza akiwamo Mohamed Salah, Roberto Firmino na Naby Keita.

Mabosi wa Barcelona wanaona hiyo ni dharau kubwa na kimekuwa kitendo cha aibu kwa sababu kila kona wanasemwa wao tu, wamekwama wapi? Sasa watawaambia nini mashabiki. Barcelona hiyohiyo ya Valverde msimu uliopita ilikumbana na tukio kama hilo la kutolewa licha ya kushinda 4-1 kwenye mechi ya kwanza. Msimu uliopita ilitupwa nje na AS Roma.

Mashabiki wamemshangaa kocha huyo kumtumia Philippe Coutinho wakati kwenye mechi ya kwanza tu alichemsha balaa, wakimshutumu hakufanya tathmini ya mechi ya mwanza kabla ya kwenda kuwakabili Liverpool Anfield. Amemweka benchi Nelson Semedo na kumwingiza baadaye sana kama alivyofanya kwa Arthur. Kwa nini hakumtumia Malcom?

Ni maswali mengi wanayojiuliza mashabiki wa Barcelona, ambao wanaamini kabisa hata rais wao, Josep Maria Bartomeu hawezi kuendelea kumvumilia kocha huyo.

Wakati stori za huko Catalan zikiwa za kocha huyo kupigwa kibuti muda wowote kutoka sasa, hii hapa orodha ya makocha wanaotajwa huenda mmoja wao akapewa bahati hiyo ya kwenda kumnoa mwanasoka bora kabisa duniani, Lionel Messi.

Quique Setien

Kocha huyu wa Real Betis ndiye anayepewa nafasi kubwa kutokana na kufundisha soka lake kwa falsafa za kupiga pasi nyingi ambalo ndilo linalotumika huko Barcelona tangu ilipokuwa chini ya Johan Cruyff. Setien ameingia kwenye ukocha baada ya kukipiga katika mechi 518 za ligi akiwa mchezaji. Baada ya kufanya vizuri kwenye kikosi cha Betis akiwa na wachezaji kama William Carvalho, Marc Bartra na Giovani Lo Celso, Setien anaweza kupata bahati hiyo ya kwenda kuinoa Barcelona.

Xavi

Kiungo gwiji huyu wa Barcelona. Xavi hivi karibuni alitangaza kustaafu soka kama mchezaji na atakachokifanya ni kuingia kwenye ukocha.

Fundi huyo wa mpira alicheza mechi 767 kwenye kikosi cha Barcelona na kushinda mataji manane ya La Liga na manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akibeba pia ubingwa wa Ulaya na Dunia akiwa na kikosi cha Hispania. Bado ameendelea kuwa kipenzi cha mashabiki huko Nou Camp, hivyo anaweza kurudi kwenda kuwanoa mastaa kadhaa kwenye kikosi hicho kama Messi ambao walikuwa wachezaji wenzake.

Max Allegri

Kocha Max Allegri ametajwa anajiandaa kuachana na Juventus mwishoni mwa msimu huu baada ya kushindwa kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya klabu hiyo kumsajili supastaa Cristiano Ronaldo.

Hakuna ubishi, Allegri amekuwa akitajwa kama mmoja kati ya makocha wenye uzoefu na uelewa mkubwa sana kwenye kazi hiyo, hivyo kuwa na huduma yake unakuwa upo kwenye mikono salama. Amekuwa na mbinu tofauti, lakini kumchukua Allegri, Barca itabili ikubaliane na jambo moja tu la kuachana na falsafa zao za kutaka kucheza soka la kuutawala mpira muda wote na pasi nyingi.

Erik ten Hag

Ajax imetolewa kiume kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, huku kocha wake, Erik ten Hag akiliweka jina lake kwenye umaarufu mkubwa huko Amsterdam, Uholanzi. Anafundisha soka lilelile alilokuwa akilitaka Cruyff na ndio utamaduni unaofanyika huko Barcelona. Tofauti ya Ten Hag ni kwamba anataka timu yake ikabe kuanzia juu na kucheza kwa haraka na hiyo iliyokana na kuchota ujuzi alipokuwa kocha wa Bayern Munich B chini ya Pep Guardiola.

Bila shaka Ten Hag hawezi kupuuzia ofa kama za Barcelona, Real Madrid au Juventus zikiletwa kuhitaji huduma yake licha ya kwamba anajiona ametulia huko Ajax.

Laurent Blanc

Kocha huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain na Ufaransa, Blanc amekuwa hana kazi kwa miaka mitatu sasa. Lakini klabu kama Chelsea na Manchester United zilikuwa zikipiga hesabu kali za kumchukua kocha huyo, hilo likiwa na maana kwamba bado anatambulika kuwa na hadhi yake huko Ulaya.

Blanc anaweza kuwa chaguo la msingi zaidi kuliko makocha wengine kwenye orodha hiyo, lakini wasiwasi uliopo ni kama ataweza kuwa na matumizi mazuri kwa wachezaji waliopo Nou Camp kwa sasa na kuwafanya wang’are au atakuwa kama Valverde tu.

Roberto Martinez

Kocha huyo Mhispaniola alifanya mambo makubwa kwenye kikosi cha Ubelgiji katika fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia na kufika hatua ya nusu fainali. Alionyesha ubora wake wa soka la klabu pia alipokuwa kwenye kikosi cha Everton.

Kuhusu kuwanoa wachezaji wenye vipaji vikubwa, Martinez amefanya kazi kubwa sana katika kikosi cha Ubelgiji kwa kuwa na wachezaji matata kama Eden Hazard, Kevin de Bruyne, Romelu Lukaku na wengine kibao ambao kimsingi wote hao wanaweza kucheza kwenye kikosi cha Barcelona na hawana tofauti na wachezaji waliopo Nou Camp kiubora.

Ronald Koeman

Kocha mwingine mkubwa kabisa huko kwenye soka la Ulaya. Koeman alikwenda kujaribu maisha kwenye Ligi Kuu England na kumshinda wakati alipokuwa katika kikosi cha Everton. Lakini, jambo hilo halina maana kwamba kocha huyo hana uwezo, kwani kwa sasa amekifanya kikosi cha Uholanzi kuwa bora kabisa na kucheza soka matata. Shida iliyopo ni kwamba Barcelona itaweza kumshawishi kumfanya Koeman aachane na soka la kimataifa na kuamua kwenda kufanya kazi huko Nou Camp licha ya kwamba ni makocha wachache sana wanaoweza kupuuza kwenda kufanya kazi na supastaa wa mpira kama Messi.

Joachim Low

Ubora wa Kocha Joachim Low hauna mashaka kutokana na kile anachokifanya huko kwenye Timu ya Taifa ya Ujerumani. Akiwa na kikosi hicho chenye mastaa kibao alibeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2014 katika fainali zilizofanyika Brazil licha ya kikosi chake hicho kwenda kuboronga huko Russia kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018.

Tatizo la Low ni moja tu kwa muda mrefu amekuwa kwenye timu ya taifa, hivyo wasiwasi uliopo kama ataweza kukimbizana na mikikimikiki ya soka la klabu ambapo mechi zimekuwa zikichezwa kila wiki na pengine kila baada ya siku tatu.

Nuno Espirito Santo

Hakuna ubishi kazi anayoifanya kocha Nuno huko kwenye kikosi cha Wolves katika Ligi Kuu England msimu huu si ya kitoto. Kocha Nuno angepata kazi ya kwenda kuinoa Barcelona pengine kitakuwa kibarua chake bora kabisa, lakini kuondoka Wolves, timu ambayo ameifanya kukamatia nafasi ya saba kwenye Ligi Kuu England msimu huu linaweza kuwa jambo gumu. Ufundishaji wake wa soka na uwezo wa kuzikabili timu vigogo huko kwenye Ligi Kuu England unaweza kuwa kigezo muhimu cha kunaswa na Barcelona kwa sababu wanahitaji kuwa na kocha mwenye mbinu za kushinda kwenye mechi ngumu na si kama alivyo Valverde ambaye amekuwa akiwapasua tu mioyo.

Leonardo Jardim

Kocha Jardim amefukuzwa kazi AS Monaco na kurudishwa. Kocha huyo alitengeneza kikosi matata kabisa cha wachezaji vijana huko Monaco kabla ya klabu kibao kuvamia kwenye timu hiyo ya kusajili wachezaji wake. Jardim alikuwa na kikosi chenye wachezaji kama Bernardo Silva, Kylian Mbappe, Benjamin Mendy, Fabinho, Thomas Lemar, Tiemoue Bakayoko na wengine, ambao waliifanya Monaco kuwa moto Ulaya na kushinda ubingwa wa Ligue 1.

Lakini wote hao waliuzwa na timu ikaanza kufanya vibaya. Kwa maana hiyo, Jardim akipata timu ambayo haina utamaduni wa kuuza wachezaji ila kununua wale waliowakali, basi ni bonge la kocha.

Antonio Conte

Ni kocha wa daraja la juu, lakini shida ni moja tu falsafa zake haziendani na Barcelona. Kocha huyo Mtaliano anapenda soka la kupaki basi, wakati Barcelona utamaduni wake ni kucheza soka la kutawala mchezo na kumiliki mpira muda mwingi. Kwa falsafa zake hizo ndio maana Conte hawezi kujihesabia kwenye orodha ya makocha wanaoweza kubamba dili la kwenda kuinoa Barcelona na ndio maana kwa sasa anafukuzia tu kibarua cha kuinoa Inter Milan, ambao wao wanahitaji matokeo zaidi kuliko kuucheza mpira. Conte yupo tu kijiweni kwa sasa tangu alipofutwa kazi huko Chelsea mwishoni mwa msimu uliopita.

Mauricio Pochettino

Tottenham Hotspur wanapambana hadi tone la mwisho la jasho kuona Pochettino anaendelea kubaki kwenye kikosi hicho hasa baada ya hiki msimu huu kuifikisha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Baada ya ushindi wa kibabe mbele ya Ajax, Pochettino aliulizwa kama anang’atuka mwishoni mwa msimu akiachana na Spurs kwenda kutafuta kazi kwingineko, kocha huyo Muargentina alicheka tu na kusema “Tusubiri tuone” jambo ambalo linaweza kuwapa nguvu Barcelona na kwenda kuilizia huduma yake kama anaweza kupatikana akachukue mikoba ya Valverde ambayo imemshinda huko Nou Camp.