KMC yaitambia Azam FC

Muktasari:

Baada ya ushindi wa Azam, KMC imeshuka mpaka nafasi ya tatu huku Azam FC wakishika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi tisa katika mechi tatu walizocheza.

OFISA habari wa klabu ya KMC, Christina Mwagala amesema licha ya klabu ya  Azam FC kuanza tambo za kukaa kileleni, wanaamini kabisa nafasi hiyo wameshikiwa wao.

 Akizungumza na Mwanaspoti akiwa mkoani Shinyanga, Christina amesema katika mchezo wao dhidi ya Mwadui wanaamini kabisa wataibuka na ushindi na kurejea katika nafasi ya kwanza.

 "Huu ni mchezo wetu muhimu na tunahitaji pointi tatu ili tuwaondoe hawa ambao wanasema kwamba wao ndio wenye Ligi kwa msimu huu huku wenye Ligi wakiwa ni KMC na wana masaa machache tu ya kukaa kileleni".

 Christina amesema katika kikosi chao wachezaji wao wote wapo vizuri na hakuna mchezaji yoyote ambaye ana majeraha hivyo wana kila sababu ya kupata ushindi.

 "Hatuna cha kupoteza katika mchezo huu zaidi ya matokeo ya pointi tatu, mashabiki wetu waje uwanjani wakiwa na amani ya kupata ushindi katika mchezo huu na wapinzani wajue kabisa hilo" alisema Christina aliyechukua nafasi ya Anuari Binde aliyemaliza mkataba katika kikosi hiko.

 Baada ya ushindi wa Azam, KMC imeshuka mpaka nafasi ya tatu wakiwa na pointi 6 katika mechi mbili walizocheza.