Juuko apewa saa 48 Msimbazi

Monday December 10 2018

 

By Thobias Sebastian

NYOTA wa Simba waliokuwa kwenye mapumziko ya siku mbili, leo Jumatatu wataendelea na mazoezi yao kujiandaa na mechi yao ya kimataifa dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia, huku beki Juuko Murshid akipewa saa 48, ili kupewa kazi nzito mjini Kitwe.

Simba itaingia kambili leo Jumatatu kabla ya Jumatano kupaa kuwafuata Mashetani Wekundu, lakini Kocha Partick Aussems akisema anampa siku mbili sawa na saa 48 ili beki huyo Mganda amridhishe ili amjumuishe kwenye kikosi kwa ajili ya mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Juuko alikosekana katika mechi mbili za raundi ya wali dhidi ya Mbabane Swallows ya eSwatini, kutokana na sababu tofauti ikiwamo kukosa maandalizi ya mchezo huo, lakini safari hii Aussems anampigia hesabu aende kumtumia Zambia.

Kocha huyo alisema anatambua uwezo wa Juuko ni bora lakini asingeweza kumuweka katika kikosi ambacho kilienda eSwatini kutokana kurudi siku chache kutoka kuitumikia Uganda.

Lakini kuelekea mechi na Nkana nafasi ya kuwa miongoni mwa kikosi kitakachoenda Zambia ipo, ila anatakiwa kufanya vizuri mazoezi ya siku mbili yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani kabla ya kupaa Zambia.

“Tunatambua tunaenda kucheza na timu yenye uwezo si ya kuibeza, hivyo mbali ya kuwa na malengo ya kushambulia lakini tunatakiwa kuwa na umakini katika kuzuia ili kutokuwapa wapinzani nafasi za kufunga,” alisema.

“Juuko ni mzuri katika kuzuia lakini hata mabeki wengine ambao wanacheza katika nafasi hiyo wapo vizuri kwahiyo yeyote atakayepata nafasi ya kutumika naimani atafanya kazi ipasavyo.

“Kikosi changu ni kizuri na tunatambua tunaenda kucheza na timu nzuri lakini mara nyingi huwa kikosi cha ushindi katika timu yoyote hakibadilikagi,” alisema Aussems ambaye alichukua mikoba ya kukinoa kikosi cha Simba kutoka kwa Pierre Lechantre.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema beki wao kisiki Juuko amebadilika si kinizamu yaani nje ya uwanja na hata ndani katika kushindania namba anapokuwa mazoezini.

“Nampongeza mno kwani siku hizi kila inapofika muda wa swala anakwenda kufanya ibada, lakini tulishindwa kwenda naye Eswatini alichelewa kurudi nchini ninaimani akifanya mazoezi vizuri tutakuwa naye katika mechi ya Nkana kule Zambia,” alisema Try Again aliyekuwa Kaimu Rais katika uongozi uliomaliza muda wake.

Mratibu wa Simba, Abbas Ally alisema; “Timu itaendelea na mazoezi Jumatatu asubuhi na safari ya kwenda Zambia itakuwa Jumatano na wapo katika hatua za mwisho kukamilisha ratiba ya muda wa kuondoka hapa nchini,” alisema.

Kama ilivyokwenda eSwatini, Simba inatarajiwa kwnda Zambia kwa tahadhari kubwa.

Advertisement