Juma Abdul, Tshishimbi ndo hivyo tena unaambiwa

Muktasari:

Kwa mujibu wa daktari wa Yanga, Shecky Mngazija wachezaji Juma Abdul na Tshishimbi majeraha yao ni makubwa huku kwa upande wa wachezaji wengine ni yake ya kawaida.

MAJERAHA yaliyowakumba wachezaji Juma Abdul na Papy Kabamba ‘Tshishimbi’ yanaweza kuiathiri timu hiyo kuelekea mchezo wao wa nusu fainali ya FA dhidi ya Simba Jumapili.

Katika mchezo huo huenda kiungo, Tshishimbi akaukosa kutokana na majeraha aliyoyapata siku chache zilizopita ambapo jana alithibitisha kwamba amegundulika kuwa na tatizo kwenye goti, ila anaomba Mungu amponye haraka.

Kwa mujibu wa daktari wa klabu hiyo, Shecky Mngazija wachezaji Juma Abdul na Tshishimbi majeraha yao ni makubwa huku kwa upande wa wachezaji wengine ni yake ya kawaida.

Alisema katika mchezo wao wa juzi dhidi ya Biashara United mjini Musoma wachezaji wake walichezewa rafu za makusudi akiwemo Haruna Niyonzima ambaye hakuweza kuendelea na mchezo huo ndani ya dakika nane tu za mchezo.

Alisema kwamba mbali na Niyonzima wachezaji wengine waliochezewa rafu katika mchezo huo ni Said Juma Makapu, Juma abdul pamoja na Kelvin Yondani.

“Yaani mchezo na Biashara kulikuwa na rafu za makusudi, wachezaji wangu wameumiaumia miguu na magoti, sasa wengine wanaendelea vizuri, tunapambana ili watumike mechi ijayo na Kagera (Sugar), ila Juma majeraha yake katika mguu yanahitaji uangalizi zaidi,” alisema na kuongeza kuwa Niyonzima aliumizwa katika goti, lakini anaendelea vizuri. Yanga inatarajia kucheza na Kagera Sugar kesho mjini Bukoba.