Julio apanga kucheza Kombe la Dunia

Saturday October 24 2020
julio pic

Kibaha, Pwani. Kocha wa timu ya Taifa chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ameweka wazi lengo lake kubwa kuwa ni kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia.

Julio amepewa jukumu la kuiongoza timu hiyo kuanzia katika mashindano ya Cecafa yanayotarajia kufanyika nchini mkoani Arusha kuanzia Novemba 10 hadi Desemba 20.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akitaja wachezaji 51 aliowaita kwa ajili ya mchujo wa awali kabla ya kupata kikosi kamili, Julio alisema furaha yake ni kuona akiivusha timu hiyo katika mashindano ya CECAFA na kwenda kwenye upande wa Afcon na aweze kwenda Kombe la Dunia kwani ndiyo furaha yake.

“Mimi ni kocha mzoefu na niliwahi kufanya kazi na kocha Kim (Paulsen) miaka ya nyuma, kwahiyo kurudi hapa ni muendelezo na nina jukumu la kupambana kuhakikisha tunamaliza nafasi mbili za juu ili kwenda Afcon kisha ndiyo tupambane tuweze kwenda Kombe la Dunia,” alisema Julio.

Alisema katika timu yake anaendeleza mfumo ambao unatumika katika kikosi cha wakubwa kwa lengo la kujenga kizazi bora kijacho. “Unajua timu hizi ndogo ndiyo msingi wa timu kubwa, kwahiyo kinachofanyika juu na chini ndiyo kiwe kile kile na ndicho tutakachofanya hata sisi.”

Kocha huyo wa zamani wa Simba na Dododa Jiji, aliongeza kuwa katika benchi lake la ufundi amemjumuisha mchezaji wa zamani Simba, Boniphace Pawasa akiamini atakuwa na mchango zaidi kwenye kuboresha vijana wake kuelekea kwenye mashindano hayo.

Advertisement

“Pawasa nimemfundisha akiwa Simba, wengine ambao nitakuwa nao watatangazwa hapo baadae.”

Julio ameita wachezaji 51, ambao atawachuja na kubakii 24, watakaokwenda kwenye mashindano ya CECAFA. Wataingia kambini Oktoba 29.

 

Advertisement