Jinsi fedha za Okwi zilivyohamishwa Simba

Muktasari:

Guhameni alidai kati ya fedha hizo zilizolipwa na Etoile, Dola 300,000 zilihamishiwa katika akaunti ya Aveva bila kujadiliwa katika kikao cha Kamati Utendaji ya Simba.

KESI inayomkabili aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva na wenzake, jana iliendelea kwa shahidi aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa klabu hiyo Amos Gahumeni, kuielezea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jinsi fedha za ada ya uhamisho wa Emmanuel Okwi zilivyohamishwa.

Shahidi huyo alieleza fedha hizo zilihamishwa kutoka katika akaunti ya klabu hiyo na kuzipeleka katika akaunti binafsi ya Aveva.

Guhumeni alitoa ushahidi huo wakati wa kesi ya Utakatishaji Fedha na kughushi nyaraka, inayowakabili Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe.

Shahidi huyo alidai, Simba ililipwa Dola za Kimarekani 319, 212 na Etoile Du Sahel ya Tunisia ikiwa ni ada ya uhamisho wa Okwi kwenda kwenye klabu hiyo ya Tunisia.

Gahumeni ambaye ni shahidi wa sita katika kesi hiyo, alieleza hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.

Guhameni alidai kati ya fedha hizo zilizolipwa na Etoile, Dola 300,000 zilihamishiwa katika akaunti ya Aveva bila kujadiliwa katika kikao cha Kamati Utendaji ya Simba.

“Fedha zilizohamishiwa katika akaunti ya Aveva ni sehemu ya fedha zilizokuwepo katika akaunti ya dola ya Simba na kwamba katika kipindi changu chote nilichokaa katika klabu ya Simba, sijawahi kuona nyaraka yoyote inayoonyesha Aveva aliikopesha klabu fedha,” alidai shahidi.

Akiongozwa na wakili wa Takukuru, Leonard Swai, shahidi huyo alidai kwa kawaida fedha zote zinazotolewa katika akaunti ya Simba kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya klabu hiyo, hujadiliwa kwanza na Kamati ya Utendaji, kabla ya kutolewa.

Alidai fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya Simba kupitia Benki ya CRDB tawi la Azikiwe na Aveva na Nyange ndio waliokuwa watiaji saini wa akaunti hiyo.

Shahidi huyo aliyeajiriwa na Simba mwaka 2014 kama Mhasibu Mkuu wa klabu hiyo alidai, Machi 14, 2016 kiliitishwa kikao cha kawaida cha Kamati ya Utendaji kilichokuwa na ajenda 10 zilizokuwa zinajadiliwa katika kikao hicho.

“Kati ya ajenda hizo 10 zilizojadiliwa, ajenda namba saba ilihusu taarifa ya mauzo ya Okwi ambaye ni mchezaji wa Wekundu wa Msimbazi na timu ya taifa ya Uganda,” alidai Guhameni, aliyekuwa na jukumu la kuandaa malipo, taarifa za fedha na kuandaa bajeti ya fedha ya mwaka.

Alidai katika ajenda namba 7, walijadili mambo matatu kuhusiana na fedha hizo na wajumbe walishauri fedha hizo zilizotolewa na Etoile, zitumuke kwa Ujenzi wa Uwanja wa klabu hiyo uliopo Bunju, Manispaa ya Kinondoni.

Pia wajumbe hao walipendekeza Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo, Hans Poppe, alipwe deni lake la Dola 17,000 na fedha nyingine wafungue akaunti maalum kwa ujenzi wa uwanja.

Aliendelea kudai, katika kikao hicho, wajumbe walikuwa tisa naye (Gahumeni) alikuwa mtu wa 10 na ndiye aliyeandika mhutasari wa kikao hicho.

“Machi 15, 2016, nikiwa ofisini nikiendelea na majukumu yangu, alikuja Kaburu (mshtakiwa wa pili) na kuniomba kitabu cha benki cha Dola ambacho kina akaunti iliyopokea fedha za mauzo ya Okwi,” alidai shahidi huyo, aliyetumia saa tatu mfululizo kutoa ushahidi wake.

Gahumeni alidai, baada ya kumpa kitabu hicho Kaburu, aliondoka nacho na alipokirudisha hakikuwa na karatasi mbili.

“Alinikabidhi karatasi ya kuhamishia fedha kutoka CRDB inayoonesha Dola 300,000, zimehamishwa kwenda akaunti ya Aveva” alidai .

Shahidi huyo alidia alipokabidhiwa karatasi hiyo aliomba apatiwe maelezo kwani hakuwa ameandika nyaraka yoyote kuhusu fedha, hivyo Kaburu alimpa maelezo aliyoyaandika kama kumbukumbu.

“Nyange alimieleza fedha hizo zimekwenda akaunti ya Aveva kwa ajili ya miradi ya klabu na fedha nyingine zitatoka kupitia bajeti itakayopitishwa na Kamati ya Utendaji.”

Alifafanua, baada ya kuandika maelezo hayo, yalisainiwa na yeye mwenyewe, Kaburu na Aveva na kimaadili hakuruhusiwa kudhibiti fedha iliyo kwenye akaunti binafsi.

“Kama Mhasibu Mkuu, siwezi kuthibiti fedha zilizokwenda katika akaunti binafsi.”

Hata hivyo baada ya kusaini maelezo, alipewa nyaraka inayohusu malipo kwa ajili ya ununuzi wa nyasi, Mkandarasi wa Ujenzi wa kiwanja hicho cha Simba ikiwa ni Kampuni ya Ranky Infrastructure & Engineering Ltd. Ililipwa Dola 50,000.

Malipo mengine ni kibali cha serikali cha ujenzi huo na klabu ililipa Dola 900, vile vile alipewa taarifa na Nyange, Dola 17,000 alizokuwa akidai Hanspope zimeshalipwa.

Shahidi huyo alibainisha kwa kipindi chote alichokuwepo Simba, hajawahi kuona nyaraka yoyote inayoonyesha Aveva aliikopesha Simba na kama mtu alikopa, lazima kuwepo makubaliano ya kukopa na kurejesha mkopo huo.

“Hivyo fedha zilizokwenda katika akaunti ya Aveva ni sehemu ya fedha zilizokuwepo katika akaunti ya dola ya klabu ya Simba Sport Klabu.”alidai Shahidi.

Imeandikwa na Hadija Jumanne, Sifras Kingamkono na Daniel Francis