Jay Msangi, promota wa ngumi asiyeishiwa mikasa

Mwenyewe anasema jina tapeli sio geni kwake. Ndilo linamtambulisha haraka kwenye ramani ya ngumi nchini, lakini anasisitiza kuwa ndiye promota anayefanya mapambano ya ngumi za kulipwa yenye mvuto nchini.

Jay Msangi, promota wa ndondi asiyeishiwa mikasa ya mara kwa mara katika mapambano anayoandaa.

Tangu aingie kwenye ndondi kwa mara ya kwanza na kuandaa pambano kubwa la ubingwa wa dunia wa WBF kati ya Francis Cheka na Phil Williams wa Marekani, Msangi amekuwa na msururu wa mikasa. “Nimekuwa ‘black listed’ lakini kwa nia mbaya, wengi wamekuwa wakinituhumu kwa vitu ambavyo sivyo,” anasema promota huyo.

Msangi anasema maono na uwezo mkubwa katika kuandaa mapambano ndiyo unamfanya kuingia kwenye matukio ya mikasa ya mara kwa mara.

Alipoingia kwenye ramani ya ndondi alifanya ‘promo’ kubwa katika mchezo huo ikiwamo kumleta bingwa wa zamani wa dunia wa uzani wa juu, Frans Botha nchini kushuhudia pambano la Cheka na Phil Williams, lakini baada ya pambano hilo aliishia kufungiwa. “Watu walijua nimeingia kutapeli, lile lilikuwa pambano langu la kwanza kufanya nchini, ugeni wa nchi ukasabababisha baadhi ya watu kunizunguka.”

Katika pambano hilo lililopigwa 2013 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, mabondia wa Tanzania akiwamo Cheka waligoma kupanda ulingoni hadi walipwe fedha.

Lilikuwa tukio lililoleta tafrani ukumbini mbele ya aliyekuwa Waziri wa Michezo, Fenella Mkangara, lakini pia Mmarekani aliondoka nchini bila kulipwa fedha zake. Msangi alifungiwa kuandaa mapambano kabla ya kukiri kosa na kulipa madeni ya pambano ikiwamo kumlipa Mmarekani na kuruhusiwa kuendelea.

Hata hivyo, licha ya kuandaa mapambano yenye mvuto na upinzani, Msangi alilalamikiwa na baadhi ya mabondia kuhusu malipo. Wengi walikiri promota huyo yuko vizuri kwenye uhamasishaji, lakini tatizo ni pesa.

Ingawa mwenyewe anadai mabondia wanaomtuhumu ni uchwara, lakini wenye viwango ambao ameingia nao mikataba anafanya nao kazi vizuri.

“Siko hivyo, nachafuliwa na washindani wangu ambao wamekuwa wakiunganisha ‘doti’ hasa baada ya kutokea ishu ya kushindwa kumlipa bondia Mmarekani aliyepigana na Cheka,” anasema. Mkasa wake mwingine uliotikisa ni ule wa Afrika Kusini alipokuwa na bondia Ibrahim Class. Katika pambano hilo la Septemba 2018 kuwania ubingwa wa mabara wa IBF, Class alichapwa na Azinga Fuzile kwa TKO, lakini alilalamika kupewa maji ambayo alidai yalimlevya raundi ya nne na kupigwa.

Bingwa huyo wa zamani wa dunia wa Global Boxing Council (GBC) alimtuhumu pia Msangi kutaka kuwadhulumu fedha.

Msangi alikiri kugoma kumpa Class fedha za pambano kwani alitaka alipwe kwanza fedha zake za uwakala Dola 1,800. “Yote hayo yalitokea baada ya Palasa (Chaurembo) kuwaleta hotelini wahuni ili wanifanyie vurugu akidai nimewatapeli fedha zao,” anasema Msangi huku Palasa akikanusha na kudai Msangi alitoa Dola 7,000 badala ya 10,000, hivyo kuhisi dalili za kutapeliwa.

Akizungumzia madai ya kumwekea Class dawa kwenye maji, Msangi anasema: “Kama ni kweli nimefanya, basi nitakuwa mafia. Class alipigwa ngumi ya pua raundi ya pili akalala chini, alihesabiwa hadi saba hakutaka hata kuamka, tulimlazimisha akaamka na kuendelea, lakini hakuwa fiti, alipigwa.” Aliporejea nchini Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), ilimfungia hadi ilipojiridhisha. Promota huyo ambaye amewahi kuandaa mapambano mengine ya Cheka na Ajetovic, Mohamed Matumla na Mthailand, Mfaume Mfaume na Habibu Pengo, Hassan Mwakinyo na Arnel Tinampay ameibuka na mkasa mwingine hivi karibuni baada ya pambano la Dullah Mbabe na Twaha Kiduku lililopigwa Agosti.

“Mapambano niliyofanya mwaka huu ndiyo namba moja nchini, lakini ajabu aliyefanya vizuri ndiye wa kwanza kufungiwa,” aneleza Msangi.

Katika mkasa huo uliosababisha Azam Media kumfungia kufanya naye kazi kama wadhamini, Msangi anakiri imetokana na pambano la Mbabe na Kiduku. “Wameniandikia barua (Azam Media), wakieleza kuna sababu ambazo hawakuridhika nazo, tulikubaliana tufanye pambano la Mfaume na Tinampay, lakini kukawa na ugumu Tinampay kuja nchini kutokana na janga la corona.”

Anasema pambano la Kiduku na Mbabe lilikuwa la utangulizi kusindikiza la Mfaume na Tinampay, lakini wakalifanya kuwa kubwa. Msangi anadai aliwaandikia Azam Media barua kuwaeleza hilo ambayo hawakuipinga na walikuwa wamempa asilimia 70 huku asilimia 30 walikubaliana baada ya pambano.

Anasema pambano hilo lilitumia fedha nyingi kuliko ambazo walipata, hivyo kusababisha baadhi ya watu kutolipwa kwa wakati. “Niliwaomba niwalipe Jumatatu (siku tatu baadaye), nilipokwenda kuomba ile asilimia 30 iliyosalia nikaambiwa imezuiwa na kuambiwa nilikiuka makubaliano ya mkataba, ndipo changamoto ilianzia hapo.”

Anasema alilazimika kulipia Uwanja wa Uhuru lilipopigwa, ingawa awali ilikuwa ni bure. Meneja wa uwanja, Gordon Nsajigwa anasema Msangi alipaswa kulipia uwanja.

Patrick Kahemele wa Azam anasema promota huyo alikiuka makubaliano ya mkataba na vielelezo vipo wazi.

Anasema awali alitaka Dola 25,000 wakashuka hadi 18,000 lakini kwa ajili ya pambano la Tinampay na Mfaume walimpa Dola 14,500 ikabaki Dola 3,500. “Tulikubaliana siku hiyo pia Twaha Kiduku na Mbabe wacheze, lakini baada ya kupewa Dola 14,500 akasema Mfaume ni mgonjwa hawezi kucheza.

“Nilimwambia tunafanya pambano hili tukimaliza tunaachana na wewe na ndicho kilitokea, baada ya pambano, Dullah Mbabe alipiga simu analalamika hajalipwa, nikasema kama mabondia hawajalipwa, basi ile Dola 3,500 izuiwe hadi awalipe,” anasema. Hata hivyo, baadaye bondia huyo alilipwa na wao walimpa Msangi fedha zilizobaki.

Kaimu rais wa TPBRC, Aga Peter ‘Mnazareth’ anasema suala la promota huyo liko Baraza la Michezo la Taifa (BMT), huku kaimu katibu mkuu wa BMT, Neema Msitha akisema hawajapokea malalamiko kutoka kwa Msangi na mdhamini wake, hivyo hawawezi kuingilia masuala binafsi.