Jamani Wanajangwani mmeyasikia ya Batigoli?

Muktasari:

  • Straika huyo aliongeza kwa kusema, ni vizuri kwa Yanga kufananikiwa kwa sababu ubora wa timu hiyo utachangia nchi kuwa na ligi bora ambayo ni muhimu kwa timu zetu katika michuano ya kimataifa.

STRAIKA wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel ‘Batigol’ amewashtua wanachama wa Yanga na kuwataka wasisinzie kipindi cha kampeni badala yake wakitumie kupima hoja za wagombea wao ili kuwapigia kura viongozi wanawafaa.

Gabriel aliyekuwa mmoja ya washambuliaji hatari nchini enzi akicheza, alisema Wanayanga wakisinzia wanaweza kujikuta wanapata viongozi wenye mawazo mgando.

“Viongozi wenye mawazo mgando wataipeleka Yanga pabaya na mwishowe mashabiki na wanachama wakajikuta hata ule upinzani baina yao na Simba unapotea,” alisema na kuongeza;

“Simba wanaweza kusajili wachezaji wazuri ambao siku zote huwa ghali na kuwalipa mishahara minono, lakini ili Yanga waendelee kuwa washindani watakiwa kuwa na watu makini watakaokuwa na mipango ya kisasa kwenye uongozi wao.”

Alisema kama Yanga watayachukulia poa maneno yake na kuyapuuza watamkumbuka pindi maji yakiwafika shingoni, huku akisisitiza anatamani kuiona Yanga ikiwa vizuri kiuchumi ili Simba iwe na mpinzani wa kweli katika Ligi Kuu.

Straika huyo aliongeza kwa kusema, ni vizuri kwa Yanga kufananikiwa kwa sababu ubora wa timu hiyo utachangia nchi kuwa na ligi bora ambayo ni muhimu kwa timu zetu katika michuano ya kimataifa.