Ishu ya Morrison, Yanga yajibu mapigo

JUZI kati kwenye Kilele cha Wiki ya Mwananchi, Yanga iliwasapraizi mashabiki wao baada ya kumtaja winga Mghana, Bernard Morrison ‘BM3’ kuwa ni kati ya wachezaji wao 28 waliosajiliwa msimu huu, lakini buana juzi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemchomoa nyota huyo katika kikosi hicho.

Katika orodha mpya ya wachezaji 2,684 waliosajiliwa msimu huu, Morrison jina lake linaonekana kwenye usajili wa klabu ya Simba na hayupo kwenye kikosi cha Yanga kilichosaliwa na wachezaji 27.

Yanga imeendelea kusisitiza Morrison ni mchezaji wao na wataenda kumdai Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo ya Kimataifa (CAS) na wamepuuza uamuzi wote ya TFF juu ya winga huyo.

Yanga imekuwa na mvutano na mchezo huo kabla ya kufikishana TFF katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ambayo baada ya kusikiliza ilimtangaza kama mchezaji huru, licha ya kukiri kuna mkataba baina yao uliobainika una upungufu.

Yanga ilidai imemuongezea mchezaji huyo mkataba wa miaka miwili, wakati mchezaji akikanusha kuwa hana mkataba na klabu hiyo zaidi ya ule wa miezi sita ambao ulikwisha.

Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alipoulizwa jana imekuwaje Morrison jina lake limeonekana Simba na halipo Yanga kama walivyoendelea kushikilia ni mchezaji wao, alisema kwa kifupi; “Tumesimamia uamuzi wa kamati yetu, ndio sababu tumeutambua usajili wa Morrison Simba.”

Hata hivyo, uongozi wa Yanga kupitia kwa Ofisa Habari wao, Hassan Bumbuli uliishangaa TFF kumpeleka Morrison Simba ikihoji imetumia vigezo gani.

“Hatujui ni kigezo gani wametumia, lakini vyovyote itakavyokuwa, bado Morrison ni mchezaji wetu na tunaamini tutapata haki yetu Cas,” alisema Bumbuli aliyesisitiza suala hilo halitaisha kirahisi kama watu wanvyofikiria.