Mashujaa yalipa kisasi, yaandika rekodi

Muktasari:

  • Mchezo huo wa mzunguko wa pili, Mashujaa FC imetakata nyumbani kupitia mabao ya Jeremanus Josephat dakika 12, Hassan Cheda (dk 22) na Reliants Lusajo (dk 60).

MASHUJAA FC wamefanikiwa kulipa kisasi mbele ya KMC FC baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Mchezo huo wa mzunguko wa pili, Mashujaa FC imetakata nyumbani kupitia mabao ya Jeremanus Josephat dakika 12, Hassan Cheda (dk 22) na Reliants Lusajo (dk 60).

KISASI KIMELIPWA
Ushindi huo ni kama Mashujaa FC imelipa kisasi baada ya kushuhudiwa mzunguko wa kwanza Desemba 2, 2023 KMC wakiwa nyumbani wakishinda mabao 3-2.

REKODI YAANDIKWA LAKE TANGANYIKA
Matokeo hayo kwa Mashujaa, ni rekodi kwao kwani tangu timu hiyo ipande daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu huu haijawahi kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao uwanja wa nyumbani.

Mashujaa ambayo katika uwanja wa nyumbani imecheza mechi 13, kati ya hizo imeshinda sita huku moja tu dhidi ya KMC ndiyo imezaa mabao mengi.

Lakini pia huo ni ushindi wa pili mkubwa katika ligi msimu huu baada ya Februari 25, mwaka huu kuifunga Geita Gold mabao 3-1 ikiwa ugenini Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita.

Mashujaa ambayo inapambana isirudi ilipotoka kwa maana ya Championship, ushindi wa leo umewafanya kufikisha pointi 26 na kupanda nafasi moja kutoka 14 hadi 13.

Kwa upande wa KMC, kichapo hicho kimewafanya kukosa fursa ya kupanda nafasi ya nne ambapo sasa imesalia na pointi zake 33 katika nafasi ya tano baada ya mechi 26 ikiachwa pointi moja na Coastal Union iliyopo nafasi ya nne na pointi 34.